Hamas kuwaachilia mateka wengine wa Israel Jumamosi
13 Februari 2025Kundi hilo limesema limedhamiria kuendelea na mchakato wa kuwaachilia mateka wote wa Israel kulingana na ratiba iliyopangwa katika makubaliano ya usitishaji wa mapigano kwenye Ukanda wa Gaza. Limeongeza kuwa wasuluhishi wa Misri na Qatar wamesema watafanya kazi kuhakikisha kuwa vikwazo vyote vinaondolewa na makubaliano ya kusitisha vita yanatekelezwa.
Awali, Hamas ilitishia kuchelewesha kuwaachilia huru mateka wa Israel likiishutumu Tel Aviv kwa kutokutimiza wajibu wake ikiwemo kushindwa kuruhusu vifaa kuingia Gaza.
Katika hatua nyingine, makumi ya matingatinga, magari yanayohusika katika ujenzi na yaliyobeba nyumba zinazohamishika yameonekana yakiwa kwenye foleni katika upande wa Misri wa kivuko cha Rafah yakisubiri kuingia Gaza. Taarifa hiyo ni kulingana na Shirika la habari la Al-Qahera lenye uhusiano wa karibu na serikali ya Misri.
Soma zaidi: Mashine nzito na nyumba zinazohamishika hazitaingia Gaza kupitia Rafah
Licha ya hilo, msemaji wa serikali ya Israel Omer Dostri ameandika kupitia ukurasa wake wa X kuwa, nyumba zisizohamishika au mashine nzito hazitaruhusiwa kuingia Gaza. Dostri ameongeza kuwa hakuna bidhaa zinazoruhusiwa kuingia Ukanda wa Gaza kupitia kivuko cha Rafah.
Kwa mujibu wa makubaliano ya sasa ya kusitisha vita, kivuko cha Rafah kimefunguliwa ili kuwapitisha wagonjwa na majeruhi. Misaada mingine inaruhusiwa pia kuingia Gaza kupitia kivuko cha Kerem Shalom.
Katika hatua nyingine, familia za mateka wa Israel wanaoshikiliwa Gaza mapema leo waliifunga barabara kuu ya Tel Aviv wakati wakitaka makubaliano ya kusitisha vita yaendelee kuheshimiwa.
Shai Moses, mpwa wa Gadi Mozes anayeendelea kushikiliwa na Hamas amenukuliwa akisema kuwa, ''Tumekuja kuwakumbusha Waisraeli waamke wawe nasi barabarani kwa sababu Waziri Mkuu wetu na serikali yetu inacheza na maisha ya watu wetu waliotekwa. Na tunapaswa kuwaokoa. Tunaitaka serikali iache kucheza na akili zetu, iache kuyahujumu makubaliano na iendelee nayo hadi yatakapokamilika.''
Familia za mateka hao zimepaza sauti baada ya hofu iliyokuwa imetanda awali kuwa makubaliano hayo yangevunjika baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump kutoa pendekezo la Marekani kuidhibiti Gaza na kuwapeleka Wapalestina mahala kwingine.