Kumbukumu ya miaka 60 tangu kushambuliwa vikali mji wa Dresden wa Ujerumani wakati wa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia.
13 Februari 2005Asubuhi ya leo kuliendeshwa misa makanisani, mashada ya mauwa yaliwekwa katika kaburi la pamoja la watu waliokufa siku hiyo na pia mbio za mshikamano wa amani zilifanywa. Wanazi mambo walikusanyika katika eneo jingine la mji na wakayaita mashambulio hayo ya mwaka 1945 kuwa ni mauaji ya kiholela kwa kutumia mabomu.
Misa ya alfajiri iliendeshwa katika kanisa la Msalaba kuwakumbuka watu waliokufa katika mji huo hapo Februari 13, mwaka 1945. Dresden ni mji ulioko katikati ya Mto Elbe na ulikuwa na unabakia kuwa ni kama lulu ya utamaduni wa Kijerumani.
Wanariadha 60, mmoja kutoka kila mwaka, walikwenda mbio kukumbuka namna mji huo uliokuwa hauna ulinzi na ambao ulisheheni watu waliokuwa wanalikimbia jeshi la Urussi lililokuwa linasonga mbele uliovoharibiwa kutokana na mabomu yalioangushwa na ndege 1,200 za Waengereza na Wamarekani.
Mwanamke mmoja aliyenusuruika na mashambulio hayo anaelezea hivi:
O-Ton::
+Nyumba yetu ilipigwa kwa mabomu mara kadhaa. Sote nyumbani tulibakia sakafuni na mume wangu akatuambia: Kunaungua, kunanuka harufu ya moto. Hapo akafungua mlango wa mwanzo na kote tukaona kunawaka moto tu. Hatujakuwa na chaguo lengine isipokuwa kuukimbia moto huo ili kuyanusuru maisha yetu.+
Mablozi wa nchi za nje, wakiwemo wale wa Uengereza na Marekani, waliweka mashada ya mauawa kuwakumbuka karibu watu 35,000 waliokufa kutokana na silaha za kemikali kama zile za Napalm. Inatazamiwa leo usiku watu 10,000 watakusanyika katikati ya mji huo, huku wakimbeba mishumaa kuukumbuka ule usiku ambapo mji wa Dresden ulichomwa.
Madhimisho ya mwaka huu yanaangaliwa kwa hamu kwa vile chama cha Wanazi mambo leo, NPD, karibuni kilishinda uchaguzi katika bunge la Mkoa wa Saxony ambao mji mkuu wake ni Dresden. Watu 2,000, wengi wao vijana waliovaa nguo nyesui walikusanyika kufanya mkutano wa hadhara, huku wakibeba bendera nyeusi, nyeupe na nyekundu na muziki wa Bach na Wagner ukisikika katika vipaaza sauti. Polisi waliweka ulizi. Baadhi ya watu hao walibeba mabango yalioandikwa HATUTASAHAU. Bango jingine liliandikwa namna hivi: Vyombo vya habari na televisheni zinaongopa.
Mauwa meupe yalisambazwa kwa watu waliokuwa wanataka kuandamana dhidi ya Chama cha NPD.
Katika taarifa iliotolewa Berlin hii leo, Kansela Gerhard Schroader alilaani kile alichokiita kuwa ni majaribio ya watu wa mrengo wa kulia sana kuiteka nyara siku hii na kuyatumia kwa maslahi yao mateso walioyapata watu. Aliahidi kuyapinga kwa njia zote majaribio hayo ya kutaka kuitafsiri historia upya. Alisema hawatastahamilia kuona sababu na matokeo yanabadilishwa. Kansela Schroader alisema maelfu ya watu wasiokuwa na hatia, wakiwemo watoto na wakimbizi wengi, walikufa katika hali mbaya sana. Moja kati ya miji mizuri kabisa ya Ulaya iliharibiwa. Alisema tunaomboleza leo na kuwakumbuka wahanga wa vita na wa utawala wa mabavu wa Wanazi katika Dresden, Ujerumani na Ulaya.
Wakaazi wa Dresden wana fahari juu ya kanisa la Fruenkirche lililoko katika mji huo na ambalo liliharibiwa kabisa mwaka 1945. Kanisa hilo limeanza kujengwa upya kwa miaka 15 sasa tangu Ujerumani iliopoungana tena mwaka 1990.
Licha ya maelfu ya raia waliouwawa mjini Dresden, karibu ya Wajerumani miilioni 15 baadae walifukuzwa kutoka Ulaya Mashariki baada ya vita vikuu vya pili vya Dunia kulipia kisasi uhalifu uliofanywa na Wanazi.
Mabigwa wanatahadharisha kwamba japokuwa kipindi cha miaka 60 huenda kikaruhusu kufanywa tena tathmini ya kina juu ya yale yaliotokea na kufanyika, hata hivyo, wahanga wa Kijerumani wasilinganishwe kabisa na karibu Wayahudi milioni sita walioangamia katika mauaji ya kiholela.
Miraji Othman