Gen-Z Kenya waandamana kuwakumbuka wenzao 60 waliouawa 2024
25 Juni 2025Hata hivyo polisi walilazimika kutumia mabomu ya kutoa machozi kuwakabili waandamanaji katika jiji la Nairobi, huku usalama ukidumishwa katika majengo ya serikali.
Anga ya taharuki na moshi ya mabomu ya kutoa machozi ilitanda katika miji ya Nairobi, Mombasa, Nakuru na maeneo mengine ya Kenya huku waandamanaji wakijitokeza kwa wingi katika siku ya kumbukumbu ya mwaka mmoja baada ya vijana wa Gen-Z kuuawa kwenye tukio la kihistoria walipolivamia bunge la taifa la Kenya.
Waandamanaji hao waliokuwa wakielekea katika kituo kikuu cha polisi cha Nairobi alikofia Albert Ojwang walikabiliwa na polisi wa kupambana na ghasia huku wakiwarushia mabomu ya machozi kuwatawanya.
Mtu mmoja ajeruhiwa kwenye maandamano
Barabara kuu za kuingia jijini zilifungwa na polisi kuwazuia waandamanaji kuingia Katikati mwa jiji. Maduka mengi yalifungwa kwa hofu ya uhalifu. Mtu mmoja amejeruhiwa kwenye vurugu hizo.
Awali katika majengo ya bunge ambapo waandamanaji 60 waliuawa mwaka uliopita usalama ulidumishwa na polisi, huku nyaya za miba zikiuzingira eneo hilo. Kiongozi wa chama cha upinzani cha Wiper, Kalonzo Musyoka pamoja na baadhi ya viongozi wa upinzani waliruhusiwa kuweka mashada ya maua kando ya barabara ya Bunge bila kukumbana na vurugu zozote.
Viongozi hao walitembea kutoka Kanisa la Holy Family Basilica, ambako walikuwa wamefanya maombi awali, lakini hawakuruhusiwa kuvuka vizuizi vya polisi. Hawakuhudhuria ibada rasmi ya kanisani bali walifanya maombi nje ya kanisa, umbali wa hatua chache kutoka Uwanja wa Bunge.
"Kutajwa kwa siku ya leo kuwa Likizo ya kuwakumbuka wahanga wa tukilo la mwaka jana, kumetokana na moyo wa uzalendo na uwajibikaji wetu na wala sio kutafuta umaarufu kama wanavyofanya wengine. Imetokana na kujitolea kwetu kwa taifa na maslahi ya wananchi,” alisema Kalonzo Musyoka.
Polisi walazimika kutumia mabomu ya machozi
Katika mtaa wa Kitengela viungani mwa jiji la Nairobi, polisi walitumia mabomu ya machozi kuwatawanya waandamanaji waliokuwa wakija jijini Nairobi kuungana na wenzao. Waandamanaji walichoma moto magurudumu barabarani na kusitisha usafiri.
Maandamano haya yanajari wakati ambapo visa vya vifo mikononi mwa maafisa wa polisi na utejakaji nyara vikiongezeka. Familia ya Mwalimu na mwanablogu Albert Ojwang' ambaye aliuawa mikononi mwa polisi inasubiri kupata haki kwa mauaji yake katika mazingira ya kutatanisha.
Polisi pia walilazimika kutumia mabomu ya machozi katika miji ya Kakamega na Kisii. Mapema Jumatano asubuhi Waziri wa Usalama wa taifa Kipchumba Murkomen alionekana Katikati ya jiji la Nairobi akiwarai wananchi kufanya maandamano ya amani.
Aidha Rais William Ruto jana Jumanne, bila kurejelea maandamano haya moja kwa moja, alisema hakuna mtu aliye juu ya sheria na kuwaonya wale ambao wanalenga kuwachokoza au kuwatishia maafisa wa usalama. Matamshi ambayo yanazidi kuibua gumzo.