Kremlin: Vitisho vya Trump havizuii mazungumzo na Ukraine
18 Julai 2025Mapema wiki hii, Trump alitangaza kwamba Moscow ina siku 50 kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano, au ikabiliwe na vikwazo vikali na ushirikiano wa kijeshi ulioimarishwa na Ukraine, kauli iliyokosolewa vikali na Wizara ya Mambo ya Nje ya Urusi, na kuitaja kama vitisho.
Msemaji wa Kremlin, Dmitry Peskov, amekosoa pia vikwazo vipya vilivyowekwa na Umoja wa Ulaya na kuitaja hatua hiyo kama sehemu ya msimamo wa "kuendelea kupinga Urusi."
"Hadi sasa, tunaona msimamo thabiti wa kuipinga Urusi kutoka Ulaya. Tumesema mara kwa mara kuwa tunachukulia vikwazo hivi vya pande moja kama visivyo halali. Tunavipinga. Wakati huo huo, tumepata kinga fulani dhidi ya vikwazo, tumejifunza kuishi chini ya vikwazo. Tutahitaji kuchambua vikwazo vipya ili kupunguza madhara yake kuwa mabaya. Zaidi ya hayo, vikwazo vipya huongeza athari mbaya kwa nchi zinazofuatilia vikwazo hivyo, ni panga lenye makali pande zote mbili."
Urusi na Ukraine zilifanya duru mbili za mazungumzo ya amani nchini Uturuki mwanzoni mwa mwaka huu ambazo zilipelekea makubaliano ya kubadilishana wafungwa na miili ya wanajeshi.
Lakini bado hakuna tarehe iliyowekwa kwa raundi ya tatu na pande hizo zinazopigana bado ziko mbali katika masharti ya kusitisha mapigano au kufikia makubaliano ya amani.