Kovu lisilofutika la mateso ya Wanazi kwa Wajerumani weusi
9 Mei 2025Uhalifu kama vile ubaguzi wa rangi, utumwa na mauaji ya halaiki dhidi ya Wayahudi, jamii za Roma, Sinti, watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja na jamii nyingine, umehifadhiwa vyema katika kumbukumbu.
Mwanahistoria Robbie Aitken, wa Chuo Kikuu cha Sheffield Hallam cha Uingereza, amefanya tafiti kuhusu jamii ya watu weusi wa Ujerumani kwa miaka 20.
Anabainisha kwamba kumekuwa na hali ya kusita kwa Ujerumani kutambua na kukubali kuwa watu weusi wamekuwa sehemu ya Ujerumani tangu mwishoni mwa miaka ya 1800.
Licha ya kuwa idadi kamili haifahamiki, maelfu ya watu wenye asili ya Afrika waliwasili Ujerumani kutoka katika maeneo kadhaa ya Africa, Caribbean, Marekani na Marekani ya Kusini.
Jamii hiyo tayari ilishatengwa kutokana na mdororo mkubwa wa kiuchumi wa mwaka 1929.
Lakini utawala wa kibaguzi wa Kinazi ulioingia madarakani mwaka 1933 ulizidi kufanya hali kuwa ngumu.
"Tunazungumza kuhusu watu waliovuka mipaka, waliohama hama sana, tunazungumzia kipindi ambacho watawala wa Kinazi wenyewe waliteketeza nyaraka kwa hiyo kupata taarifa lilikuwa jambo gumu." anasema Mwanahistoria Robbie Aitken
Kulingana na mwanahistoria Robbie Aitken wakati utawala wa kinazi wa Ujerumani ulipoingia madarakani, yeyote aliyetaka kuwa mbaguzi, yeyote aliyekubaliana na mitazamo yao angeweza kuyasema hayo yote mitaani na kuwanyanyasa watu kwa maneno na hata kimwili. Walikuwa na uhuru wa kufanya hivyo.
"Baadhi ya familia zilifukuzwa kwenye makazi yao ili kutoa nafasi kwa watu wanaounga mkono Wanazi au wanachama. Baadhi ya Wajerumani weusi wenye biashara zao walilengwa waziwazi"
Wanazi waliwadunisha watu weusi kote Ujerumani
Maelfu ya watu weusi walionekana kuwa duni. Utawala huo wa kibaguzi wa Ujerumani kuanzia mwaka 1933 hadi 1945 chini ya Adolf Hitler ulitumia sheria na sera za kibaguzi kudidimiza nafasi za kiuchumi na kijamii kwa watu weusi walioishi Ujerumani.
Hitler aliwalenga watoto wenye mzazi mmoja mwafrika na mwingine mweupe walioishi katika eneo kando ya mto Rhine mashariki mwa Ujerumani.
Watoto hao walifuatiliwa kimya kimya kupitia askari wa wa kikosi maalumu waliofahamika kama Gestapo na kisha waliwahasi ili wasipate nafasi ya kuzaliana.
Chapisho muhimu lililotolewa lililopewa jina "Showing Our Colors. Afro-German Women Speak Out," liliwakilisha wakati muhimu kwa jamii ya watu weusi nchini Ujerumani.
Kitabu hicho kinaonesha tathmini ya kihistoria, mahojiano, shuhuda binafsi na ushairi unaoweka wazi ubaguzi nchini Ujerumani.
Mwanahistoria wa Ujerumani Katharina Oguntoye anasema historia ya Wajerumani wenye asili ya Afrika inapaswa kupewa nafasi hasa kwenye mitaala mashuleni.
Kwa sasa mapambano ya kutaka kutambuliwa kwa madhila ya watu weusi na uhalifu dhidi yao enzi za utawala wa Kinazi bado hayajazaa matunda na kizazi kipya hakina budi kushindana na jamii ya ujerumani inayoelekea kuegemea siasa kali za mrengo wa kulia.