Korea yabomoa kituo cha kuzikutanisha familia za K. Kusini
13 Februari 2025Msemaji wa wizara ya Korea Kusini ya masuala ya muungano amesema kubomolewa kwa Kituo cha Kuzikutanisha Familia cha Mlima Kumgang ni hatua isiyo ya kiutu ambayo inahujumu matakwa ya familia zilizotenganishwa.
Korea Kusini imeelezea kusitikishwa na hatua hiyo na kuhimiza kusitishwa mara moja kwa ubomoaji huo.
Afisa kutoka Jumuiya ya Familia Zilizotenganishwa za Kikorea amelaumu kuzorota kwa mahusiano kati ya Korea mbili chini ya Rais aliyeondolewa madarakani Yoon Suk Yeol kuwa sababu ya kubomolewa kituo hicho. Mamilioni ya watu walitenganishwa na Vita ya Korea ya 1950-53, ambayo iliigawanya rasi hiyo.
Tangu mwaka wa 1988, karibu Wakorea Kusini 130,000 wamezisajili familia zao zilizotenganishwa. Kufikia mwaka wa 2025, karibu watu 36,000 bado wako hai, kwa mujibu wa takwimu rasmi.
Asilimia 75 ya familia zilizotenganishwa zinasema hazifahamu ikiwa jamaa zao wako hai au walikufa.