Korea Kusini: Ndege yawaka moto kwenye uwanja wa Busan
29 Januari 2025Abiria wote 169 na wahudumu saba waliokuwemo ndani ya ndege hiyo walifanikiwa kutoka nje kwa kutumia milango ya dharura. Shirika la habari la Korea Kusini Yonhap limesema watu watatu walipata majeraha madogo.
Ndege hiyo ilikuwa ya shirika la ndege la Korea Kusini la Air Busan. Sehemu ya nyuma iliwaka moto huku picha zikionyesha miali ya moto kutoka kwenye paa la ndege hiyo. Ilikuwa imewasili Busan ikitokea Hong Kong.
Haikufahamika kama moto uliwaka kabla au baada ya kutua. Tukio hilo limejiri baada ya ajali mbaya kabisa katika historia ya safari za anga nchini Korea Kusini mwezi mmoja tu uliopita. Ndege ya abiria ya Shirika la Ndege la Korea Kusini la Jeju Air iliubamiza ukuta baada ya kutua katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Muan. Karibu abiria wote 181 waliokuwemo walikufa katika ajali hiyo ya mwishoni mwa Desemba.