Korea Kusini: Mahakama yamrejesha madarakani Han Duck-soo
25 Machi 2025Han alishika nafasi hiyo baada ya Rais Yoon Suk Yeol kuondolewa madarakani kutokana na kutangaza sheria ya kijeshi mwezi Desemba mwaka jana, hatua iliyosababisha mgogoro mkubwa wa kisiasa nchini humo.
Katika hukumu yake, mahakama hiyo ilipiga kura 7-1 kutengua uamuzi wa bunge, ikieleza kuwa matendo ya Han hayakukiuka uaminifu wa umma na hivyo hayakustahili kumuondoa madarakani. Mara baada ya hukumu hiyo, Han alirejea kazini na kutoa ujumbe wa umoja kwa taifa.
Katika hotuba yake kwa taifa, Han alisema: "Nitazingatia maslahi ya taifa lote na watu wetu na kusikiliza kila sauti ili taifa letu lisonge mbele katika zama za busara na mantiki. Ninaomba kwa dhati ushirikiano kutoka pande zote za kisiasa ili taifa letu lishinde mgogoro huu na kusonga mbele kwa maendeleo.”
Aidha, Han aliongeza kuwa kipaumbele chake kikubwa ni kukabiliana na changamoto za kiuchumi, hasa mvutano wa kibiashara duniani, ambao umeongezeka kufuatia kuingia madarakani kwa Rais wa Marekani Donald Trump.
Soma pia: Mahakama yatoa waranti ya kukamatwa rais wa Korea Kusini
Alisisitiza akisema: "Kufuatia kuingia madarakani kwa Rais Trump, mvutano kati ya Marekani na China umeongezeka, na sasa tunakabiliwa na mabadiliko makubwa ya kijiografia na mpangilio mpya wa uchumi duniani. Kama Kaimu Rais, nitafanya kila niwezalo kuhakikisha utawala thabiti kwa mujibu wa sheria na katiba, na nitatumia juhudi na ujuzi wangu wote kulinda maslahi ya taifa katika vita hivi vya kibiashara vinavyoendelea.”
Hatma ya Rais Yoon Suk Yeol bado kitendawili
Uamuzi huu wa mahakama umetolewa wakati taifa likiwa limegawanyika kisiasa huku maandamano makubwa yakiendelea, yakijumuisha wanaomuunga mkono Rais Yoon na wale wanaompinga.
Kesi dhidi ya Rais Yoon imekuwa ikisubiriwa kwa muda mrefu zaidi katika historia ya mahakama hiyo, na ikiwa ataondolewa rasmi madarakani, taifa hilo litalazimika kufanya uchaguzi mpya wa urais ndani ya siku 60.
Soma pia:Mahakama ya Katiba ya Korea Kusini kuamua hatma ya Rais Yoel
Wachambuzi wa kisiasa wanasisitiza kuwa uamuzi huu dhidi ya Han haumaanishi moja kwa moja kuwa mahakama itachukua mwelekeo gani katika kesi ya Rais Yoon. Hata hivyo, uamuzi huo umeimarisha ari ya wafuasi wa Yoon na kuongeza shinikizo dhidi ya wapinzani wao kisiasa.
Kwa upande mwingine, wabunge wa upinzani walioanzisha mchakato wa kumwondoa Han madarakani wanakosolewa kwa hatua yao ambayo imetajwa kuchochewa na siasa, na hivyo kusababisha taifa kukosa uongozi thabiti kwa kipindi kifupi.
Kurejea kwa Han ofisini kumeongeza wito wa maridhiano na utulivu wa kisiasa huku taifa hilo likiendelea kusubiri kwa hamu uamuzi wa mwisho kuhusu hatma ya Rais Yoon.