Korea Kusini kufanya uchaguzi wa mapema kumchagua Rais mpya
8 Aprili 2025Korea Kusini itafanya uchaguzi wa Rais wa mapema tarehe 3 Juni kumchagua Rais mpya atakayechukua nafasi ya Yoon Suk Yeol, kiongozi aliyenyang'anywa madaraka kutokana na amri yake ya kijeshi aliyoitoa nchini humo mwaka jana.
Rais anayekaimu Han Duck-soo ametoa tamko hilo siku nne baada ya majaji wa mahakama ya katiba nchini Korea Kusini kukubaliana kwa kauli moja kuondolewa kwa Yoon kutoka madarakani. Hatua hiyo kwa mujibu wa katiba ya Korea Kusini ni lazima ifuatiwe na uchaguzi ndani ya kipindi cha siku 60. Rais mpya atakayechaguliwa atatumikia kwa kipindi cha miaka mitano madarakani.
Soma zaidi: Manusura wa mauaji ya Rwanda waomba Burundi, DRC na Ubelgiji zishitakiwe
Wakati huo huo vyama vya siasa nchini Korea Kusini vinatarajiwa kuanza harakati za kuwachagua wagombea wa urais watakaoviwakilisha vyama vyao.
Katika chama cha Yoon cha PPP waziri wa kazi Kim Moon Soo mfuasi mkubwa wa Yoon Suk Yeol ni miongoni mwa wagombea wanaopewa kipaumbele. Mgombea mwingine anayepewa nafasi ya mbele ni meya wa zamani wa jiji Seoul, Se-Hoo.