Korea Kaskazini yathibitisha kupeleka wanajeshi Urusi
28 Aprili 2025Shirika la habari la Korea Kaskazini, KNCA, limeripoti kwamba wanajeshi wa Pyongyang waliisaidia Moscow kulirejesha eneo lililokuwa chini ya udhibiti wa Ukraine katika mpaka wa Urusi ulioko kwenye mkoa wa Kursk.
Hatua hiyo inakuja siku chache baada ya Moscow kuthibitisha ushiriki wa Korea Kaskazini. Rais Vladimir Putin wa Urusi mapema hii leo alinukuliwa akiusifia ujasiri wa wanajeshi hao wa Korea Kaskazini.
Korea Kusini na mashirika ya kijasusi ya Magharibi kwa muda mrefu yameripoti kwamba Pyongyang ilipeleka zaidi ya wanajeshi 10,000 kuisaidia Urusi kwenye mkoa huo wa Kursk.
Kulingana na ripoti ya Tume Kuu ya Kijeshi ya Pyongyang, uamuzi wa kiongozi wa taifa hilo Kim Jong Un wa kupeleka wanajeshi, ulikuwa ni kwa mujibu wa mkataba wa ulinzi baina ya mataifa hayo.