Kongo yawarejesha Wamarekani waliokuwa wamehukumiwa kifo
9 Aprili 2025Msemaji wa rais wa Kongo Tina Salama amesema watu hao watatu watatumikia vifungo vyao nchini Marekani kufuatia kurejeshwa kwao kulikofanikishwa na Ubalozi wa Marekani. Ofisi ya rais imesema Wamarekani hao waliondoka Kongo jana Jumanne asubuhi. Masharti ya makubaliano ya kuwahamisha wafungwa hao hayakufahamika wazi. Hii ni siku chache tu baada ya hukumu zao za kifo kubadilishwa na kuwa za maisha jela.
Miongoni mwa Wamarekani hao watatu ni Marcel Malanga mwenye umri wa miaka 21, mtoto wa kiongozi wa upinzani Christian Malanga, aliyeongoza jaribio hilo lililozimwa la mapinduziambalo liliilenga ikulu ya rais mjini Kinshasa. Baba yake aliuawa wakati akipinga kukamatwa, kw amujibu wa maafisa wa Kongo. Marcel Malanga alisema baba yake alimlazimisha kushiriki katika tukio hilo.
Kurejeshwa huko kumejiri huku kukiwa na juhudi za mamlaka za Kongo kutia saini mkataba wa madini na Marekani ili nayo ipewe msaada wa ulinzi utakaoisaidia Kinshasa kupambana na waasi mashariki mwa nchi hiyo.