Kongo yapiga marufuku ndege za Rwanda kutumia anga yake
12 Februari 2025Serikali ya Kongo imechukua uamuzi huo jana Jumanne na kueleza kuwa ndege zote za kiraia na za serikali zilizosajiliwa Rwanda au kwingineko lakini zenye makao yake nchini Rwanda sasa zimepigwa marufuku kuruka juu ya anga ya DRC, hii ikiwa ni kutokana na vita vya kichokozi vilivyosababisha vifo vya watu 3,000 huko Goma.
Wachambuzi wanasema hatua hii itakuwa pigo kwa Rwanda kutokana na ukubwa wa anga ya Kongo, lakini wakahoji ni namna gani serikali ya Kinshasa itaweza kutekeleza hatua hiyo. Hasa ikizingatiwa kuwa mwishoni mwa mwaka 2024, taarifa za Umoja wa Mataifa zilieleza kuwa Rwanda ilivuruga mawasiliano ya anga huko mashariki mwa Kongo , na hivyo kuhatarisha maisha ya abiria waliopanda ndege za kibiashara eneo hilo.
Hayo yakiarifiwa mapigano yanaendelea kati ya jeshi la Kongo FARDC na waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda. Kwa sasa makabiliano yameripotiwa huko Ihusi wilayani Kalehe katika jimbo la Kivu kusini ambako nia ya waasi hao ni kuutwa mji wa Bukavu baada ya kuchukua udhibiti wa mji wa Goma.
Juhudi zaendelea kuutafutia suluhu mzozo huo
Siku ya Jumatatu, kufuatia ombi la maaskofu, rais wa Kongo Felix Tshisekedi alikutana na wawakilishi wa Baraza la Kitaifa la Maaskofu wa Kongo na Kanisa la Katoliki (CENCO-ECC) wakiongozwa na Kadinali Fridolin Ambongo na walijadiliana kuhusu hali ya usalama na kibinadamu mashariki mwa DRC.
Viongozi hao wa Kanisa Katoliki nchini Kongo waliwasilisha mapendekezo ya kuumaliza mzozo huo waliyoyaita "mkataba wa kijamii kwa ajili ya amani", ambapo miongoni mwa mambo mengine wanaitaka serikali kukaa meza moja na M23, jambo ambalo limepingwa vikali na serikali ya Kinshasa ikiwataka kwanza viongozi hao wa kidini kukemea uvamizi unaofanywa na nchi jirani ya Rwanda kama alivyoelezea Patrick Muyaya, msemaji wa serikali ya Kongo:
" Kabla sijazungumzia hatua hii ya viongozi wa Kanisa, ukweli ni kwamba raia wa Kongo 3,000 wameuawa katika mazingira mabaya. Hao walikuwa ni waumini wao, lakini hadi sasa sijasikia viongozi wa dini wakikemea hilo waziwazi. Kwa sababu kama upo kwenye nyumba inayoungua, jambo la kwanza ni kufikiria namna ya kuuzima moto huo. Kwa hiyo hatua yao ya kwanza ingelikua kukemea uovu unaofanywa na nchi jirani ambayo sote tunaifahamu."
Soma pia: Wanajeshi wa Kongo waliokimbia mapigano kupandishwa kizimbani
Hali ya kibinaadamu inaendelea pia kuwa mbaya. Umoja wa Mataifa umesema watu 110,000 wamelazimika kuhamishwa huko Mashariki mwa Kongo baada ya M23 kuamua kuzifunga kwa nguvu kambi za wakimbizi. Kulingana na Jukwaa la Mashirika ya Kimataifa yasiyo ya Kiserikali, uasi wa M23 mashariki mwa Kongo umepelekea kuhamishwa kwa takriban watu 500,000.
(Vyanzo: Mashirika)