Kongo yakanusha M23 kuwakamata wapiganaji wa FDLR
3 Machi 2025Kundi la waasi la M23 mwishoni mwa juma lilitoa taarifa ya kuwakamata wapiganaji wa kundi la wanamgambo wa kihutu la FDLR. waliohusika katika mauaji ya Watutsi nchini Rwanda mnamno mwaka 1994.
Waasi wa M23 walienda mbali na kutoa video ikionesha ikiwakabidhi wapiganaji 20 wanaodaiwa kuwa wa FDLR kwa mamlaka ya Rwanda makabidhiano yaliyofanyika kwenye moja ya kituo cha mpakani baina ya nchi hizo mbili.
Kaimu Msemaji wa M23 Oscar Balinda amesema wataendelea na msako zaidi ili kuwatia nguvuni na kuleta hakikisho la kile alichokiita usalama katika maeneo hayo.
"Kitakachofuata ni kwamba tutaendelea kuwasaka waasi waliojificha katika jiji la Goma. Kila siku tumekuwa tukipata taarifa juu ya ukosefu wa usalama, na taarifa za kusikika milio ya risasi na mengineyo."
Taarifa ya jeshi la Kongo imesema tukio hilo ni la kubuni na lilikuwa na lengo la kulidhihaki jeshi la Kongo na kuongeza kwamba kusambaa kwa video hiyo ni sehemu ya mkakati wa Rwanda kuhalalisha kile walichokiita uvamizi katika maeneo ya kimkakati nchini humo.
Soma pia:DRC: M23 yawarejesha waasi wa FDLR nchini Rwanda
Katika ufafanuzi wake zaidi kwa umma taarifa hiyo ilisema kwamba, wale wanaoonekana kwenye video hiyo ni wafungwa wa zamani wa kundi la FDLR ambao walichukuliwa na kuwaoneshwa kama wapiganaji wa kundi hilo waliokamatwa hivi karibuni mjini Goma.
Aidha jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limelishutumu jeshi la Rwanda kwa uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu kwa kile ilichokisema "iliwanyonga" askari waliojeruhiwa katika uwanja wa mapambano na wagonjwa katika moja ya hospitali mjini Goma.
Mzozo katika eneo hilo umeendelea kuzusha hofu ya kuzuka kwa vita ya kikanda, vikihusisha nchi kadhaa ikiwemo Rwanda na Uganda.
Uganda yapeleka wanajeshi mashariki mwa Kongo
Siku ya Jumapili jeshi la Uganda lilithibitisha kuwapeleka wanajeshi wake katika eneo jingine la kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kupambana na makundi yanayomiliki silaha.
Msemaji wa masuala ya ulinzi katika jeshi la Uganda Felix Kulayigye amesema askari wake wameingia katika mji wa Mahagi na tayari wamechukua udhibiti.
Hatua ya jeshi la Uganda ni kufuatia ombi la jeshi la Kongo baada ya kuwepo kwa madai ya mauaji ya raia takriban 51 yaliyofanywa na kundi la wapiganaji la CODECO.
Ikumbukwe kwamba Uganda ina maelfu ya wanajeshi katika jimbo la Ituri chini ya makubaliano na serikali ya Kongo.
Wachambuzi wanahofia kuwa kuongezeka kwa uwepo wa vikosi vya Uganda na Rwanda mashariki mwa DRC kunaweza kusababisha kujirudia kwa kile kinachoitwa Vita vya Pili vya Kongo vilivyodumu kuanzia mwaka 1998 hadi 2003, na kuhusisha mamilioni ya vifo na majanga mengine ikiwemo njaa na magonjwa.