Kongo yakanusha madai ya M23 ya kuwanasa wapiganaji wa FDLR
2 Machi 2025Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limekanusha hii leo Jumapili kwamba wapiganaji 20 wanaohusishwa na mauaji ya halaiki ya Rwanda walikamatwa katika ardhi yake, na kuitaja video inayoonesha wapiganaji hao wakikabidhiwa kwa Rwanda kuwa ni ya kutengenezwa.
Kauli hiyo imekuja baada ya kundi la M23 linaloungwa mkono na Rwanda kusema jana Jumamosi kwamba limewakamata wapiganaji wa kundi la kihutu la Democratic Forces for the Liberation of Rwanda (FDLR),waliohusika katika mauaji ya Watutsi nchini Rwanda mwaka 1994.
Soma zaidi: Jiji la Hamburg kupiga kura leo, SPD inatarajiwa kushinda
Rwanda kwa muda mrefu imekuwa ikisisitiza uwepo wa FDLR mashariki mwa Kongo ili kuhalalisha uungaji mkono wake kwa M23, kundi ambalo limeteka maeneo mengi ya mashariki mwa Kongo ikiwa ni pamoja na miji mikuu ya majimbo ya Goma na Bukavu.
Kongo pia imeishutumu M23 kwa kufanya mauaji ya wanajeshi waliojeruhiwa na wagonjwa katika hospitali mjini Goma na kusema kwamba vitendo hivyo ni uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu. Mzozo huo wa mashariki mwa Kongo unazidi kuongeza hofu ya kuwa unaweza kusambaa na kuwa mzozo wa kikanda.