Kongo yaitaka Rwanda kulipa fidia ya vita
12 Februari 2025Katika shauri hilo Kongo imeiomba mahakama kuibana Rwanda kuwajibika kwa uharibifu iliousababisha ikiwa ni pamoja na kulipa fidia.
Leo ikiwa ni siku ya kwanza ya kusikilizwa kwa shauri hili la Congo ambalo litasikilizwa kwa siku mbili, waleta maombi Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo pamoja na mambo mengine wameiambia mahakama hiyo kuwa uharibifu ambao Rwanda imeufanya, unahusisha mzozo wa silaha uliodumu tangu mwaka 2021 eneo la mashariki mwa Congo, kati ya vikosi vyake vya jeshina kundi la waasi la M23 linalodaiwa kuungwa mkono na Rwanda.
Mbele ya jopo la majaji, Waziri wa Sheria na Mwanasheria Mkuu wa Rwanda Dr. Emmanuel Ugirashebuja, ameiomba mahakama hiyo kutupilia mbali madai ya Congo kwakuwa hoja zake haziendani na mikataba ya kimataifa iliyoridhiwa na Rwamba, na kwamba Mahakam hiyo haina haki kisherika ya kusikiliza shauri hilo.
Ameiambia DW kwamba "mahakama inayo mamlaka maalumu, huwezi kupoteza muda wa mahakama au muda wa jamhuri ya Rwanda kwa kuleta madai ambayo mahakama haina uwezo wa kuyasikiliza, ndio maana tumebishana sana kuhusu mamlaka ya mahakama. Kimsingi mahakama hii haina mamlaka ya kusikiliza madai yaliyowsilishwa na Congo.”
Rwanda: Mgogoro hauhusishi masuala ya haki za binadamu
Rwanda inasema kuwa kulingana itifaki ya Mahakama ya Afrika ya haki za binadamu na watu, Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi inayohusiana na mgogoro wa kati ya yake na Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, kwakuwa mgogoro huo, hauhusishi moja kwa moja masuala ya haki za binadamu ya wananchi wa Rwanda au Congo.
Jopo la wanasheria wa Rwanda wameiambia mahakama kuwa, kesi hiyo inahusisha masuala ya mizozo ya kijeshi na siasa za kikanda.
Rwanda ikifafanua zaidi iliongeza kwamba mizozo hiyo ni nje ya wigo wa mamlaka ya mahakama hiyo.
Upande wa waleta maombi Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, unasema madai ya Rwanda yanapotosha sheria na itifaki ya Mahakama, na inapaswa kuwajibishwa kwa makossa iliyoyafanya. Samwel Mbemba Kabuya ni wakili upande wa waleta maombi.
"Kesi hii ni muhimu kwetu Congo kutokana na machafuko yaliyotokea, vifo vya mamilioni ya watu na machafuko yanayoendelea mpaka sasa. Tunataka Mahakama ichukue hatua kwa Rwanda, wawajibike kwa makossa waliyoyafanya na haya mambo yasitokee tena.”
Kesi hii namba saba ya mwaka 2023, inatarajiwa kusikilizwa tena Kesho ambapo mahakama itatoa maamuzi dhidi ya madai ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo. V