DRC yaanza harakati za kumwondolea kinga ya kisheria Kabila
1 Mei 2025Waziri wa Sheria Constant Mutamba, amesema tayari Mwanasheria Mkuu wa Jeshi ameshaliomba Baraza la Seneti la Kongo kubatilisha kinga ya kutoshtakiwa aliyonayo Kabila kutokana na nafasi yake kuwa seneta wa maisha.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Kinshasa, Waziri Mutamba amesema Kongo imekusanya ushahidi wa wazi kuhusu uhalifu wa kivita, uhalifu dhidi ya ubinadamu na mauaji ya halaiki ya raia wasiyo na hatia pamoja na maafisa wa jeshi dhidi ya Rais huyo wa zamani. Amesema Kabila anapaswa kurejea Kongo ili ajibu madai hayo mbele ya sheria la sivyo kesi yake inaweza kuendeshwa bila uwepo wake.
Soma zaidi: Serikali ya DRC yasimamisha shughuli zote za chama cha Kabila
Licha ya tamko hilo lililotolewa Jumatano jioni, kufikia Alhamisi bado haijawekwa wazi kama kuna nyaraka zozote zitakazokuwa tayari kusainiwa ili kufanikisha kuondolewa kwa kinga ya Kabila ifikapo Ijumaa.
Joseph Kabila, aliyekubali kuondoka mamlakani mwaka 2018 baada ya karibu miongo miwili ya utawala wake, amekuwa nje ya nchi tangu mwishoni mwa mwaka 2023 na mara nyingi amekuwa nchini Afrika Kusini. Mwezi uliopita alisema angerejea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ili asaidie kupata suluhisho la mgogoro wa mashariki mwa taifa lake ambako waasi wa M23 wameyateka maeneo makubwa.
Wasiwasi wa kukwama juhudi za Marekani katika kuutatua mzozo mashariki mwa Kongo
Kurejea Kongo kwa Kabila ambaye amekanusha kuwaunga mkono waasi hao, kunaweza kutatiza juhudi za Marekani za kuukomesha uasi katika eneo la Mashariki linalokabiliwa na mzozo. Eneo hilo lina madini ya thamani ambayo utawala wa Rais Donald Trump umedhamiria kusaidia kuyachimba.
Duru za habari ziliashiria kuwa Rais huyo wa zamani angewasili au tayari alishawasili Kongo, kwenye mji wa mashariki wa Goma ulionyakuliwa na waasi hao wanaoungwa mkono na Rwanda mapema mwaka huu.
Hivi karibuni, Wizara ya mambo ya ndani iliziisimamisha shughuli za chama chake cha People's Party for Reconstruction and Democracy (PPRD), siku kadhaa baada ya mali zake kushikiliwa na maafisa wa usalama.
Katibu Mkuu wa chama hicho Ferdinand Kambere amesema jaribio la kumwondolea kinga Rais wa zamani Joseph Kabila linaonesha kuwa serikali inahofia kurejea kwake. Kambere amemnyooshea kidole cha lawama Rais Felix Tshisekedi ambaye ni hasimu wa Kabila kuwa ndiye chanzo cha mzozo wa Mashariki mwa Kongo.