Ukatili wa kijinsia waongezeka kwa kiasi kikubwa DRC
2 Julai 2025Kusonga mbele kwa waasi wa M23 kuelekea mji wa Bukavu mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kuligeuza vijiji kadhaa kando ya Ziwa Kivu kuwa maeneo ya vita kati ya Januari na Februari.
Katika vijiji vya kaskazini mwa jimbo la Kivu Kusini, wanawake na watoto walikumbwa na vitendo vya ubakaji na ukatili wa kingono kutoka kwa wanaume waliokuwa na silaha.
Makundi ya kijamii na wanaharakati wanalilaumu jeshi la Kongo pamoja na wapiganaji wa kundi la Wazalendo (kutoka Kivu Kaskazini) kushiriki katika matukio haya. Ingawa wanashirikiana na jeshi la taifa kupambana na waasi wa M23, baadhi ya wapiganaji wamehusishwa na uhalifu huu.
Waathirika wakosa haki
Miongoni mwa waathirika ni Riziki (jina limebadilishwa kwa usalama wake), ambaye aliileza DW jinsi askari watatu walivovamia nyumba yake na mmoja wao kujaribu kumbaka.
"Alikuja hadi chumbani kwangu lakini nilijitetea. Wenzake walimuita waondoke lakini alikataa, akisema anataka kunibaka. Kwa bahati nzuri mwanangu alinisaidia na wakaondoka baada ya kuharibu kila kitu,” anasema Riziki.
Tukio hilo lilitokea Februari katika kijiji cha Kavumu, kilomita 30 kutoka Bukavu. Tangu wakati huo, Riziki, mama wa watoto watano, alikimbilia Bukavu kutafuta usalama na haki kupitia kesi ya mfano iliyopangwa.
Lakini hali ilibadilika ghafla baada ya M23 kuuteka mji wa Bukavu. Majaji, mawakili, washitakiwa na hata baadhi ya waathirika walilazimika kukimbia.
Riziki anasema, "Nilianza biashara ndogo, lakini baadaye wanaume wenye silaha walivamia tena mtaa niliokimbilia na kuua majirani wawili. Nimerudi hivi karibuni.”
Hofu na aibu zatatiza utoaji wa taarifa
Katika maeneo yaliyotekwa na M23, kama Bukavu na Goma, mashuhuda wameripoti ongezeko la ubakaji – hasa dhidi ya wake za watu na wasichana – ambapo baadhi ya wanawake hulazimishwa kufanya ngono ili kupata huduma fulani. Waathirika wengi hawaripoti kutokana na hofu au aibu.
Mfano ni msichana mmoja aliyeshitakiwa kimakosa na jirani yake na kuwekwa rumande na Idara ya Usalama. Akiwa huko, alikumbwa na tukio la kutisha: "Usiku mmoja askari aliyekuwa zamu alinitishia kunibaka.
Nilipomkataa, alinipiga. Nilipiga kelele na mkuu wake akaja. Walichapwa viboko. Niliambiwa hili ni jambo la kawaida kwa walinzi hao,” alisimulia kwa DW.
Ubakaji kama silaha ya vita
Ingawa hakuna takwimu rasmi kwa ukanda huu, ripoti ya shirika la Madaktari Wasio na Mipaka (MSF) inaonyesha kuwa tangu kuanza kwa mapigano kati ya jeshi la Kongo na M23, matukio ya ukatili wa kingono yameongezeka kwa kasi, hasa Kivu Kaskazini.
Mnamo 2024, karibu waathiriwa 40,000 walihudumiwa na MSF, na kati ya Januari hadi Aprili 2025, waathriwa na manusura 7,400 waliripotiwa. Kaskazini mwa Kivu Kusini, MSF imewahudumia karibu wahanga 700 tangu mwanzo wa mwaka.
"Matumizi ya ubakaji kama silaha ya vita ni mkakati wa kuvunja jamii,” anasema Amadou Bocoum, mkurugenzi wa Care International nchini DRC.
Ripoti ya Care inaeleza visa 67,000 vya ukatili wa kingono dhidi ya wanawake na wasichana ndani ya miezi minne ya kwanza ya mwaka – ongezeko la asilimia 38 ukilinganisha na mwaka uliopita.
Ukosefu wa msaada wa dharura – Marekani yalaumiwa
"Kadri mapigano yanavyoendelea, ndivyo wanawake wengi wanavyojeruhiwa na kubakwa,” anasema Bocoum. "Lakini serikali ya Marekani imepunguza ufadhili – ambao hufikia asilimia 40. Hatuna tena dawa za dharura za kuzuia maambukizi ya VVU baada ya ubakaji katika vituo vyetu.”
Willermine Ntakebuka kutoka shirika la Vision Communautaire anasema: "Huu ni mwaka wa 30 wa vita – ni muda mrefu mno kwa wanawake na wasichana kuendelea kubeba gharama za migogoro.”
MSF inaeleza kuwa mashambulizi mengi yamefanyika kwa kutumia silaha na waathirika hawawezi kuwatambua wahalifu kwa sababu ya kuwepo kwa watu wengi waliokuwa na silaha – raia na wanajeshi.
Kongo si pekee, Sudan na Ethiopia pia waathirika
Kongo ni mfano mmoja tu wa mateso yanayowakumba wanawake na wasichana barani Afrika. Ripoti ya Amnesty International ya Aprili 2025 inaeleza unyanyasaji wa kijinsia uliotekelezwa na vikosi vya Rapid Support Forces (RSF) nchini Sudan kati ya Aprili 2023 na Oktoba 2024.
"RSF imewashambulia wanawake na wasichana kwa ukatili wa kutisha,” anasema Deprose Muchena wa Amnesty.
Watu 30 walihojiwa, wengi wao wakiwa manusura waliokimbilia kambini nchini Uganda. Wote waliwatambua RSF kuwa wahalifu na kueleza madhara makubwa waliopata kimwili, kiakili na kijamii.
Nchini Ethiopia, wakati wa vita vya Tigray vilivyoanza 2020, vikosi vilitumia ubakaji, utumwa wa kingono na ukeketaji kama silaha.
Amnesty ilibaini haya katika ripoti yake ya 2021, ikionyesha jinsi wanawake na watoto walivyoteseka mikononi mwa wapiganaji.