Kongo na Rwanda: Hatua mpya ya amani yakiongozwa na Marekani
27 Juni 2025Duru za kuaminika zimeiambia DW kwamba rasimu ya makubaliano itakayotiwa saini leo, inatarajia usitishaji haraka wa mapigano. Kinshasa na Kigali wanatakiwa kutofanya mashambulizi tena, iwe ya moja kwa moja au kupitia makundi ya wapiganaji wanayoyaunga mkono. Nchi hizo mbili pia zinatakiwa kutatua tofauti zao kwa njia za amani.
Makubaliano hayo yanazungumzia pia suala la makundi ya waasi, hasa wapiganaji wa FDLR na AFC/M23, nchi hizo mbili zinajitolea kutotoa tena msaada wowote kwa makundi hayo.
Kongo na Rwanda wamekubaliana kuwasaka, ikiwezekana kwa pamoja, waasi wa FDLR huko mashariki mwa Kongo. Hata hivyo suali ni kubwa ni uwezekano wa operesheni hiyo ya pamoja wakati ambapo maeneo waliopo waasi hao kwa sehemu kubwa yanadhibitiwa na kundi la waaasi la AFC/M23.
Kwa mujibu wa rasimu ya mkataba huo, serikali ya Kongo inatakiwa kuendelea na mazungumzo ya moja kwa moja na waasi wa AFC/M23, ambayo yalianzishwa mwezi machi huko Doha, nchini Qatar.
Christian Moleka, mtaalamu wa siasa ya Kongo amesema changamoto ni ufuatiliaji na utekelezaji wa mkataba huo wa Washington.
"Tatizo sio kutia saini mkataba huo lakini utekelezaji wake. je, kuna nia nzuri ya kisiasa kati ya pande hizo mbili ?Huu sio mkataba wa kwanza wa aina hiyo kati ya nchi hizi mbili. Lakini mara hii wahusika wako tayari kujenga amani ya kudumu ? Je, mifumo ya ufuatiliaji itafanya kazi kwa ufanisi tofauti na ilivyokuwa zamani ili kusaidia utekelezaji wa makubaliano haya?", alihoji Moleka.
Maslahi ya Marekani
Moleka ameamini kwamba shinikizo la Marekani linaweza kufanikisha makubalaino ya hivi sasa. Amesema hakikisho kubwa ya kufanikisha makubalaino hayo ni msukumo wa kiuchumi wa Marekani ambayo inataka madani ya Kongo.
Kwa upande wao mashirika ya kiraia ya Kongo yanaelezea wasiwsai wao kuhusu makubalano hayo ambayo hayajazingatia hasa sababu za msingi za machafuko huko Kivu. Steward Muhindo ni muachama wa kundi la vijana wanaotaka mageuzi LUCHA.
"Kama makubalano hayo hayalazimishe jeshi la Rwanda na waasi wa AFC/M23 kuondoka katika maeneo wanayoyamiliki, kama hayaruhusu haki itandeke kwa waathiriwa wa vita, kama hayasaidie uongozi bora nchini Kongo, inamaanisha makubalaino hayo hayatachangia kurejesha amani na usalama wa kudumu mashariki mwa Kongo", alisema Muhindo.
Duru za upatanisha zinasema makubaliano hayo yanatakiwa kutekelezwa mnamo kipindi cha miezi mitatu. Na kando ya hafla hiyo waziri wa mambo ya nje wa Kongo, Therese Kayikwamba atakuwa na mashauriano na mwenzie wa Marekani Marco Rubio, kabla ya mkutano na waadishi habari.