Kongo na M23 walaumiana baada ya mazungumzo ya amani kukwama
8 Agosti 2025Katika tamko hilo la kanuni zilizotiwa saini tarehe 19 Julai katika mji mkuu wa Qatar, pande hizo mbili ziliazimia kuanza mazungumzo ya amani ifikapo Agosti 8. Hata hivyo, hadi jana, hapakuwa na dalili ya kuanza kwa ufanisi wa mazungumzo hayo Ijumaa (08.08.2025). Alhamisi, AFC/M23 ilikuwa imetangaza tayari kwamba wajumbe wake walikuwa hawajaenda Doha.
Ujumbe wa serikali ya Kongo ulikuwa ungali bado mjini Kinshasa hadi asubui yaleo. Kwa upande wa AFC/M23, msimamo unaonekana kuwa mkali zaidi: wawakilishi wao walifika Alhamisi mjini Bukavu.
Ujumbe wa AFC/M23 umedai kwamba utarejea kwenye mazungumzo huko Doha ikiwa wafungwa wao waliozuiliwa na serikali ya Kongo wataachiliwa. Lakini serikali ya Kongo inaamini kwamba bado haujafika wakati wa kuwaachilia wafungwa hao, na kwamba hatua hii ni suala la mazungumzo yanayotarajiwa kufanyika moja kwa moja.
Wakati huo huo, takriban watu wanne wamepoteza maisha katika mapigano makali yaliyoripotiwa tangu Alhamisi katika maeneo ya Walungu na Kabare katika jimbo la Kivu Kusini kati ya wapiganaji wa AFC/M23 na Wazalendo.
Kule Walungu, mapigano hayo yamefanyika haswa katika vijiji vilivyoko kati ya eneo la Walungu/Centre na Kaniola na huko Kabare mapigano yamefanyika katika vijiji vinavyopatikana kati ya Kavumu na mbuga ya wanyama ya Kahuzi-Biega.
Baraza jipya la mawaziri bila vigogo wa upinzani
Mick Mutiki ni mwanaharakati wa Shirika la raia katika Jimbo la Kivu kusini, anazitaka pande zote kuweka kando hali yakujipendelea ubinafsi na kuendelea na mazungumzo hayo kwa maslahi ya wakongo.
"Tunachokiona sio cha kutia moyo. kila wakati inaturudisha kwenye mapigano tu ijapokuwa tulipoona saini tofauti huko Washington na Doha, tulianza kutumaini kwamba hatimaye tutapumua sasa lakini!!", amesikitika Mutiki.
Haya yakijiri, Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Félix-Antoine Tshisekedi alitangaza muundo mpya wa serikali ya Kongo inayoongozwa na waziri Mkuu Judith Suminwa yenye mawaziri hamsini na tatu, dhidi ya ile yazamani iliyokuwa na mawaziri hamsini na nne. Ingawa mawaziri kadhaa wanahifadhi nyadhifa zao, marekebisho yamefanywa, na sura mpya zimejiunga na serikali hiyo.
Mfano ni waziri mkuu wazamani Adolphe Muzito aliyetajwa kwenye Wizara ya Bajeti, Floribert Anzuluni aliyeteuliwa kusimamia Mtangamano wa Kikanda, Guillaume Ngefa kwenye wizara ya sheria, huku Marie Niangé Ndambo akiwajibika kwa Mazingira.
Julie Mbuyi ataongoza Wizara Maalum ya nyazifa, Micheline Ombahe anateuliwa kwa Jinsia, Familia na Watoto, Grace Emi Kutinho anakuwa Waziri wa Vijana, na Eliezer Ntambwe ameteuliwa kuwa Waziri Mjumbe wa Ulinzi na Masuala ya Wanajeshi wa zamani.
"Ni serikali ya watu wamoja"
Albert Matabaro ni msemaji wa chama cha upinzani cha ECIDé cha Martin Fayulu katika jimbo la Kivu kusini, anasema hatarajiye mabadiliko yoyote kufuatia Serikali hiyo :
"Sisi hatugemee kitu chochote sababu ni serikali inayoundwa na walewale ambao hawajali maslahi ya raia. Martin Fayulu hakukubali kuwa mwanachama wa serikali hiyo, kwa hivyo itashindwa muda sio mrefu", alisema Matabaro.
Wakongo wengine wanaamini kwamba ilikuwa ingekuwa heri kusubiri matokeo ya mazungumzo ya sasa kati ya AFC/M23 na serikali ya Kongo au mazungumzo mengine yanayotarajiwa chini ya uongozi wa maaskofu wa kanisa katoliki na kiprotestanti ECC-CENCO nchini Kongo ili kuunda serikali ya umoja wa kitaifa.