Kongo: CODECO yashambulia raia na kuuwa zaidi ya watu 35
11 Februari 2025Kiongozi wa kundi la Djaiba katika vijiji vya Djugu Jean Vianney amesema wanamgambo wa CODECO walitekeleza shambulizi hilo ambalo lilianza majira ya saa mbili usiku, wakiwauwa wakaazi kwa kuwapiga risasi na kuziteteteza nyumba zao kwa moto.
Vianney amesema "tumewahesabu zaidi ya watu 35 waliokufa majira ya asubuhi hii leo, na juhudu za kutafuta wahanga zikiendellea." Alisema.
Aidha aliongeza kwamba wapo watu waliojeruhiwa vibaya, wengi wamepoteza maisha kutokana na kuungua na moto ndani ya nyumba zao.
Ama katika upande mwingine kiongozi wa asasi za kiraia katika eneo hilo Jules Tsuba amesema miili 49 ilipatikana hadi kufikia asubuhi ya leo Jumanne, katika wakati ambapo bado juhudi za kutafuta waathirika zaidi zikiendelea kuchukuliwa.
Soma zaidi:Duru zasema Afrika Kusini imetuma wanajeshi zaidi Kongo
CODECO ni moja ya makundi mengi ya wanamgambo yanayopigania ardhi na rasilimali mashariki mwa Kongo.
Umoja wa Mataifa umewahi kuwashutumu kwa mashambulizi dhidi ya jamii nyingine, ikiwemo wafugaji wa Hema, mashambulizi yanayoweza kuhesabiwa kama uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu.
Wengi wa waathirika katika mkasa huo kwa mujibu wa kiongozi wa Djaiba ni pamoja na watu wa jamii ya Hema, huku akiongeza kwamba mashambuliozi hayo yamefanyika wakati ambapo wanajeshi wa Kongo pamoja na walinda amani wa Umoja wa Mataifa wakiwa umbali wa takriban kilometa tatu, hivyo hawakupata masaada wa haraka.
Jeshi la Kongo pamoja na ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani hawakuzungumzia mkasa huo.
Afrika Kusini yatuma wanajeshi na vifaa zaidi Kongo
Wakati hayo yakiendelea duru za kisiasa na kidiplomasia zinaripoti kwamba Afrika kusini imetuma zaidi wanajeshi pamoja na zana za kijeshi kuelekea mashariki mwa Kongo katika siku za hivi karibuni, ikiwa ni mwezi mmoja tu baada ya wanajeshi wake 14 kuuwawa katika mapigano na waasi wa M23.
Hatua hiyo ya Afrika Kusini inachukuliwa huku kukiwa na wasiwasi kwamba mapigano Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yanaweza kuzusha vita kamili katika eneo hilo ambalo katika miaka mitatu iliyopita limeshuhudia mauaji ya halaiki, migogoro ya mipakani na hata kuongezeka kwa ukiukwaji wa haki za binadamu.
Hata hivyo Msemaji wa Jeshi la Afrika Kusini na mwenzake wa Kongo walikataa kuthibitisha kwa shirika la habari la Reuters juu ya kupelekwa zaidi vifaa vya kijeshi pamoja na askari.
Wanajeshi 84 wa Kongo wafikishwa mahakamani
Wakati hayo yakiendelea hapo jana Mamlaka nchini Kongo iliwafikisha mahakamani wanajeshi wake 84 wakituhumiwa kwa kwa mauaji, ubakaji na uhalifu mwingine dhidi ya raia katika eneo lililokumbwa na vita la mashariki.
Soma zaidi:Wanajeshi 84 wa Kongo wanaotuhumiwa kwa mauaji wapandishwa mahakamani
Wanajeshi hao wanashutumiwa kwa kuvunja nyumba za raia katika vijiji kadhaa vya maeneo ya Kabare na Kalehe katika jimbo la Kivu ya Mashariki mwishoni mwa juma, wakiwabaka wanawake kadhaa na kuua takriban watu 12. Pascal Mupenda muathirika na wakili alisema nje ya mahakama.
"Wanajeshi wote hawa tayari wameuwa watu 12, ambao vifo vyao kwakweli vinasikitisha na kumekuwa na visa vingi vya ubakaji, uporaji na wizi ndio maana wamefikishwa mbele ya sheria leo."
Asasi za kiraia ziliomba mahakama kutoa adhabu ya kifo kwa washtakiwa wote. Ikumbukwe kwamba Kongo iliondoa usitishwaji wa zaidi ya miaka 20 wa huku ya kifo mnamo mwezi Machi, uamuzi uliokosolewa vikali na wanaharakati wa haki za binadamu.