KOMBE LA TAIFA LA UJERUMANI (DFB POKALE)-KOMBE LA KLABU BINGWA BARANI AFRIKA.
23 Septemba 2004MICHEZO
Kinyan’ganyiro cha duru ya pili kati ya wiki hii cha kuania Kombe la Taifa la Ujerumani-DFB Pokale, kilipita kwa msangao kabla jioni hii Bundesliga-Ligi ya Ujerumani kurudi uwanjani huku Wolfsburg na sio mabingwa Bremen , Bayer Leverkusen wala Bayern Munich wanaoshika usukani wa Ligi.
Mabao 2 ya haraka aliotia stadi wa Paraguay Nelson Valdez, yaliwapa mabingwa watetezi Werder Bremen ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Bayer Leverkusen .Bremen ilitwaa msimu uliopita vikombe vyote viwili-Kombe la Ligi na la taifa.
Werder Bremen,wameitimua nje Bayer Leverkusen,timu iliotamba hivi karibuni tangu katika Bundesliga hata katika Champions League walipoizaba tangu Bayern Munich hata Real Madrid kila moja mabao 3:0.Lakini walipokumbana juzi na mabingwa Bremen, hawakufua dafu.
Schalke ikicheza na mzaliwa wa Ghana na mchezaji wa taifa wa Ujerumani Asamoah,iliipiga kumbo Kaiserslauten kwa mabao 4-3.Bao la ushindi la Schalke, lilitiwa na Mbrazil,Lincoln ambae msimu uliopita tu akiichezea Kaiserslauten.
Hertha Berlin,imeaga Kombe hili la shirikisho la dimba la Ujerumani, kwa kupigwa kumbo na klabu ya daraja ya tatu Eintracht Brainschweig tena kwa mabao 3-2.Timu ya daraja ya pili ya Alemannia Aaachen iliocheza finali ya kombe hili msimu uliopita ilizimwa jana duru ya pili tu ya Kombe hili na timu ya wasiolipwa ya Bayern Munich.
Borussia Dortmund iliichapa Unterhaching mabao 3:1 shukurani kwa mabao 2 maridadi ya mbrazil Ewerthon.
FC Cologne, ilioteremshwa daraja ya pili ilikumbana jana na Hansa Rostock ya daraja ya kwanza.Ikiongoza Cologne 2:1,Rostock licha ya kucheza na wachezaji 10,ilisawazisha 2:2 na mwishoe mikwaju ya penalty ikaamua hatima ya Cologne.Hansa iliibuka mshindi kwa mabao 7:5.
Shabiki mmoja –kijana wa miaka 18 alifariki dunia uwanjani kabla kipindi cha mapumziko kutokana na pigo la moyo.
KOMBE LA KLABU BINGWA:
Klabu ya ESPERENCE ya Tunisia ,inatumai kukata tiketi kesho ya nusu-finali ya Kombe la klabu bingwa barani Afrika ikipambana nyumbani na SuperSport United ya afrika Kusini.kwani ushindi kesho utawahakikishia Esperence nafasi katika hatua hiyo ya juu ya Kombe hili.Licha ya kutamba katika mashindano ya ubingwa ya tunisia mnamo mwongo mmoja uliopita, Esperence haikuweza kutwaa ubingwa wa Afrika zaidi ya mara moja.
Nafasi ya pili ya nusu-finali inaaniwa kati ya USMA ya Algeria na Jeanne d’ Arc ya Senegal .
Etoile du sahel timu nyengine ya Tunisia na Enyimba ya Nigeria -–abingwa watetezi ndio wanaotamba katika kundi A.
Bakili Bullets ya Malawi wana miadi na etoile du Sahel huko Sousse,Tunisia wakati Enyimba waweza kuitimua tena africa sports baada ya kuizima kwa mabao 3:0 katika duru ya kwanza.
Kwahivyo, ushindi wa nyumbani utazihakikishia Etoile na Enyimba nafasi katika nusu-finali.Enyimba ilipokonywa kati ya wiki hii ubingwa nyumbani Nigeria, inataka kuwa klabu ya kwanza kutetea taji lake hili baada ya Engelbert ya jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo kuweka rekodi hiyo kwa ushindi 1967 na 1968.
Mfalme wa dimba wa Brazil,Pele, atakaetimiza umri wa miaka 64 mwezi ujao ameanza utaratibu wa kudai malipo yake ya uzeeni-hii ni kwa muujibu wa shirikisho la dimba la Brazil-CBF lilivyoarifu leo.
Pele alifunga mkataba wake wa kwanza wa kucheza dimba na klabu ya SANTOS hapo 1956 au 1957 na hakuichezea klabu nyengine yoyote nchini Brazil isipokua Santos.Pele alicheza nchi za nje alipovaa jazi ya Cosmos NY kuanzia 1974.Kwahivyo, ameshachangia miaka 17 katika mfuko wa bima ya kustaafu kama inavyotakiwa kwa mchezaji nchini Brazil.
Zimbabwe ilijipatia kocha mpya kati ya wiki hii nae ni Charles Mhlauri.Mhlauri ameteuliwa wiki 3 kabla Zimbabwe kukumbana na Angola katika changamoto ya kanda ya Afrika ya kuania tiketi ya Kombe lijalo la la dunia litakalochezwa hapa Ujerumani 2006.
Mhlauri ni kocha 3 wa Zimbabwe mwaka huu na anajaza pengo lililoachwa na Rahman Gumbo alietimuliwa baada ya Zimbabwe kuzabwa mabao 3-0 na Nigeria na miezi 3 tu baada ya kuchukua nafasi ya Sunday Marimo.Zimbabwe inakumbana pia na Zambia, hapo Oktoba 24 katika changamoto ya nusu-finali ya kombe la COSAFA-Kombe la shirikisho la dimba Kusini mwa Afrika.