Kocha Xabi Alonso kuondoka Leverkusen mwisho wa msimu
9 Mei 2025Kocha wa Bayer Leverkusen Xabi Alonso anaondoka klabu hiyo baada ya msimu huu kukamilika, kabla kuhamia Real Madrid. "Huu ndio wakati muafaka kutangaza habari hii," kocha huyo raia wa Uhispania amesema Ijumaa kabla kile kinachoonekana kuwa ni mechi yake ya mwisho nyumbani katika dimba la BayArena siku ya Jumapili. "Uwazi ni mzuri kwa kila mtu"
Kocha huyo wa umri wa mika 43 amefikisha mwisho uvumi na tetesi za wiki kadhaa kwa kuwafahamisha wachezaji wake kabla mazoezi ya Ijumaa kwamba anaondoka, mwaka mmoja kabla mkataba wake kufika mwisho 2026.
Alonso, mchezaji wa zamani wa Real Madrid, aliiongoza Bayer Leverkusen kushinda taji la Bundesliga na kombe la shirikisho la Ujerumani DFB Pokal msimu uliopita baada ya kuchukua mikoba na kuiongoza timu iliyokuwa katika eneo la kushuka daraja mnamo Oktoba 2022.
"Nafikiri tunaweza kufurahi, tunaweza kuwa na fahari kwa kile tulichokifanikisha wakati wa kipindi hiki," Alonso alisema.
Wirtz kukosa mechi ya ligi ya mabingwa na Bayern
Timu yake ya Leverkusen inabaki timu pekee kukamilisha msimu wa Bundesliga bila kupoteza mechi hata moja. Hata hivyo, kilikuwa kibarua kipevu kurudia matokeo hayo msimu huu.
Leverkusen ilipoteza taji kwa Bayern Munich wikendi iliyopita huku zikiwa zimesalia mechi mbili kukamilisha msimu. "Nimejaribu kuwabana kadri inavyowezekana. Walinipatia mambo mengi sana, kwa hiyo pengine hatuna kitu sasa hivi," Alonso alisema kuwahusu wachezaji wake.
Kibarua cha Leverkusen kilikuwa cha kwanza kwa Alonso katika usimamizi wa timu kubwa baada ya taaluma yake nzuri ya kutandaza soka na Real Madrid, Liverpool na Bayern Munich.
Alitumia muda wa miaka mitatu kama kocha wa timu ya akiba katika klabu ya Real Sociedad, klabu yake nyingine ya zamani. Alianza taaluma ya ukocha katika timu ya vijana ya Real Madrid.