MichezoUhispania
Flick ammwagia sifa Lamine Yamal
1 Mei 2025Matangazo
Kocha wa Barcelona Hansi Flick amemwagia sifa Lamine Yamal baada ya kufunga goli maridadi kabisa lililonusuru kikosi hicho ambacho hatimaye kilitoka sare ya mabao 3-3 dhidi ya Inter Milan katika mkondo wa kwanza wa nusu fainali za Ligi ya Mabingwa Ulaya jana usiku.
Lamine aliyecheza mechi yake ya 100 akiwa na umri wa miaka 17, anakuwa mchezaji mdogo kabisa kufunga bao kwenye nusu fainali ya Champions na kuipiku rekodi ya Kylian Mbappe aliyekuwa na miaka 18 alipofikia mafanikio kama hayo mwaka 2017.
Goli la Yamal lilirejesha matumaini kwa Barcelona iliyokuwa nyuma kwa mabao 2-0, mwanzoni mwa kipindi cha kwanza na kuendelea kuisumbua safu ya ulinzi ya Inter Milan, hatua iliyomfanya Flick kushindwa kujizuia kummwagia sifa kinda huyo.