Kiongozi wa Waislamu wa Ismailia Aga Khan afariki dunia
5 Februari 2025Aliyekuwa kiongozi wa kiroho kwa mamilioni ya waumini wa Kiislamu wa madhehebu ya Shia ya Ismailia, Aga Khan amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 88. Wakfu wa Aga Khan umetangaza kupitia tovuti yake kwamba Karim al-Hussaini, imam wa 49 wa waumini milioni 15 wa Madhehebu hayo ya Ismailia amefariki jana Jumanne akiwa amezungukwa na familia yake huko Lisbon, Ureno.
Aga Khan alizaliwa Uswisi mwaka wa 1936. Imam huyo, mwanahisani na mfanyabiashara mwenye mafanikio makubwa alikuwa na uraia wa Uswisi, Uingereza, Ufaransa na Ureno. Alikuwa mfanyabiashara mwenye mafanikio na anayeheshimika sana, hata kuandaliwa karamu ya heshima ya chakula cha jioni na Malkia wa Uingereza Hayati Elizabeth II katika Kasri la Buckingham mnamo 2008.
Malkia Elizabeth alimchukulia kama kiongozi wa nchi. Julai, 1957 Malkia alimpa cheo cha "Mtukufu", ikiwa ni wiki mbili baada ya kifo cha babu yake Aga Khan III na kumfanya yeye sasa kuwa mrithi wa familia ya nasaba ya miaka 1,300 na kuwa kiongozi wa madhehebu ya Kiislamu ya Ismailia.
Mwanamfalme wa Wales, William na mkewe Catherine pia waliwahi kukutana na Aga Khan katika hafla iliyofanyika huko London mwaka 2019. Wawili hao walitembelea Kituo cha Aga Khan kilichopo katikati mwa London, ambako walikutana na viongozi maarufu na wafanyabiashara wenye asili ya Uingereza na Pakistan, wanamuziki, wapishi wakubwa na wasanii.
Atakumbukwa kwa kusaidia shughuli za maendeleo
Aga Khan, akisukumwa na utajiri uliomzunguka, alianza kwa kuzindua wakfu uliojikita kwenye maendeleo mnamo 1967 uliolenga kuinua viwango vya kusoma na kuandika katika nchi 18 kote katika eneo la Kusini na katikati mwa Asia, Afrika na Mashariki ya Kati.
Lakini nchini Pakistan alikumbana na changamoto kutoka kwa wanamgambo wa Taliban wa madhehebu ya Sunni waliomshutumu kwamba shule za taasisi yake zinawapotosha wanaume na wanawake nchini humo, ili wajitenge na Uislamu.
Katika ujana wake alikuwa na ndoto ya kuwa mbunifu, kabla ya kuhitimu kutoka Chuo Kikuu cha Harvard na shahada ya historia ya Kiislamu. Pia alitekeleza lengo lake la kuelimisha ulimwengu kuhusu utajiri wa utamaduni wa Kiislamu.
Watu maarufu watuma salamu za rambirambi
Watu mbalimbali wameanza kutuma salamu za rambirambi kufuatia kifo hicho. Mshindi wa Tuzo ya Kimataifa ya Amani ya Nobel Malala Yousafzai ameandika kupitia mtandao wa X ametuma salamu za pole kwa familia ya Khan pamoja na wapendwa wao wote. Ameandika Roho yake impumzike kwa amani. Ameongeza kuwa urithi wake utaendelea kuishi kupitia kazi kubwa aliyoifanya kwenye sekta ya elimu, afya na maendeleo kote ulimwenguni.
Salamu pia zimeendeleea kutolewa na viongozi kote ulimwenguni. Mfalme Charles wa III wa Uingereza amesema amesikitishwa sana na kifo cha Aga Khan, ambaye alikuwa ni rafiki yake wa karibu kwa miaka mingi, hii ikiwa ni kulingana na duru za kifalme. Chanzo hicho kimesema, hii inaeleweka kwa sababu Charles alikuiwa na mawasiliano binafsi na familia ya Aga Khan.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres pia amesema amesikitishwa sana na taarifa hizo za kifo cha Aga Khan, IV. Amesema alikuwa ni taswira ya amani, uvumilivu na upendo katikati ya ulimwengu wa sasa wenye changamoto nyingi. Amepeleka pole kwa familia yake na jamii nzima ya Ismailia.
Wakfu wa Aga Khan umesema mrithi wake atatajwa baadae.