Kiongozi wa upinzani Tanzania asema hawatosusia uchaguzi
13 Februari 2025Amesema badala yake kitahakikisha uchaguzi huo hautafanyika endapo hakutakuwa na mageuzi wanayoyashinikiza kwenye mfumo wa uchaguzi.
Akizungumza na waandishi habari mjini Dar es Salaam, Lissu amesema CHADEMA kitaishtaki serikali ya Tanzania kwa wananchi, jumuiya ya kimataifa na viongozi wa kidini ili kushinikiza mabadiliko ya katiba na sheria za uchaguzi alizosema kila wakati zinachangia kufanyika uchaguzi usiozingatia misingi ya demokrasia.
Lissu aliyechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa chama hicho Januari 22 amesema mifumo ya uchaguzi Tanzania inadhibitiwa na Rais wa nchi hiyo na kwa upande wa Zanzibar pia inadhibitiwa na Rais wa visiwa hivyo.
Amesema mfumo huo wa uchaguzi umesababisha Tanzania kuongozwa na viongozi ambao hawakuchaguliwa kwa njia halali miaka ya hivi karibuni.