Kiongozi wa upinzani Chad ahukumiwa miaka 20 jela
12 Agosti 2025Hukumu hii inatolewa wakati ambapo Chad inazongwa na misukosuko ya kisiasa tangu kutokea kwa kifo cha Idriss Déby Itno, baba wa rais aliyeko madarakani Mahamat Idriss Déby.
Shirika la kimataifa la kutetea haki za binaadmau la Human Rights Watch, limesema kuwa hukumu hiyo iliyotolewa tarehe 9 mwezi huu wa Agosti ni hitimisho la kesi inayoaminika kuwa na misingi ya kisiasa.
Succes Masra, kiongozi mkuu wa upinzani, ni mkosoaji mkubwa wa Rais Mahamat Idriss Déby. Mahakama ya uhalifu mjini N'Djamena ilimkuta Masra na hatia kwa kusambaza ujumbe wa chuki na ubaguzi kupitia majukwaa ya mtandaoni baada ya mapigano kuwaua watu 42 katikati ya mwezi wa Mei mjini Mandakao katika jimbo la Logone, eneo la kusini magharibi.
Mashirika ya haki hayajaiona hukumu
Kulingana na mkurugenzi wa shirika la Human Rights Watcheneo la Afrika ya Kati, Lewis Mudge, mahakama hazipaswi kutumika kama vyombo vya unyanyasaji wa kisiasa na kwamba hukumu ya Masra inayoashiria kufikisha ujumbe wa hofu kwa wakosoaji. Kadhalika, hilo linaashiria kuwa serikali ya Chad imeshindwa kuvumilia wakosoaji na upinzani wa kisiasa.
Human Rights Watch imebainisha kuwa haijaiona hukumu yenyewe ila wamewasiliana na waliokuwepo mahakamani wakiwemo mawakili wa Masra. Ifahamike kuwa aghalabu vita kati ya jamii za wafugaji na wakulima vimeshuhudiwa kusini mwa Chad, ila vurugu zimeongezeka katika muda wa miaka michache iliyopita na kusababisha maafa.
Masra, ambaye alikanusha mashtaka dhidi yake pamoja na watu wengine 74 Kwa kushiriki kwenye mauaji ya Mandako. Kiasi ya tisa kati ya washtakiwa hao waliachiliwa huru ila waliosalia nao pia walihukumiwa kifungo cha miaka 20 jela. Mahakama pia iliwatoza faini ya dola milioni 1.8 za Marekani. Mawakili wa washtakiwa wote wameapa kukata rufaa katika Mahakama ya Juu.
Kabla ya uchaguzi mkuu kufanyika mwezi Mei 2024, Masra na wafuasi wa upinzani wa Chama cha The Transformers, walihangaishwa na kuteswa na uongozi wa muda wa rais wa wakati wa kipindi hicho cha mpito.
Ghasia za kisiasa zaizonga Chad
Mwishoni Mwa Februari, rais wa Chama cha kisoshalisti kilicho na mipaka, Yaya Dillo, aliuawa na vikosi vinavyoaminika kuwa vya usalama waliposhambuliwa mjini N'Djamena kwenye makao yao makuu. Kufikia sasa mauaji yake hayajathibitishwa rasmi.
Ghasia zilizo na misingi ya kisiasa zimeizonga Chad hasa baada ya maandamano kufanyika Oktoba 2022 kuadhimisha siku ambayo jeshi liliahidi kuachia madaraka na kuukabidhi mikoba ya uongozi serikali ya kiraia. Uongozi huo wa kijeshi ulishika hatamu kufuatia kifo cha rais wa zamani wa Chad, Idriss Déby Itno mwaka 2021.
Itakumbukwa kuwa kiongozi wa upinzani Succès Masra alikimbilia uhamishoni kufuatia maandamano hayo, ila alirejea baada ya juhudi za upatanishi zilizoongozwa na Rais Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, kama msuluhishi wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Mataifa ya Afrika ya Kati, ECCAS.