Kiongozi wa Syria awataka Waalawi kuweka chini silaha
8 Machi 2025Shiraa ametoa onyo hilo kwenda kwa makundi ya wapiganaji wa kabila la Alawi baada ya kutokea makabiliano kati yao na vikosi vya utawala mpya wa Syria.
Makabiliano hayo yalizuka baada ya wapiganaji wa kabila hilo kufanya mashambulizi yanayotajwa kuwa ndiyo makubwa zaidi yakiilenga serikali mpya ya Syria tangu ulipoangushwa utawala wa Bashar al-Assad, Disemba mwaka jana.
Katika kujibu mashambulizi hayo, hapo jana vikosi vya Syria vilivamia vijiji kadhaa vya jamii ya Waalawi na "kuwaua" watu 162 . Taarifa hizo zimetolewa na Shirika linalofuatilia haki za binadamu nchini Syria.
Hadi kufikia sasa zaidi ya watu 300 wamekufa tangu makabiliano yalipozuka kwenye jimbo la pwani ya Bahari ya Mediterania la Latikia, magharibi mwa Syria ambalo ndiyo makao ya jamii ya Alawi iliyokuwa nguzo ya utawala wa Assad.
Hapo kabla wafuasi wa Assad waliwashambulia na kuwaua askari polisi 16. Hiyo ilikuwa ni katika kujibu mashambulizi ya vikosi vya usalama vya Syria yaliyosababisha mauaji ya wanamgambo 28 na raia wanne.
Mashambulizi yaliyopangwa kwa ustadi yatishia uthabiti wa Syria
Mustafa Kneifati, afisa wa usalama wa Latakia, amesema shambulizi hilo lilipangwa kwa ustadi mkubwa na makundi kadhaa yenye silaha yanayomuunga mkono Assad, na lilivilenga vituo vya ukaguzi na maafisa waliokuwa kwenye doria huko Jableh.
Kneifati amesema vikosi vya usalama vinafanya kazi ya ziada kuwaondoa wapiganaji hao, na kwamba watarejesha hali ya usalama na utulivu katika jimbo hilo na kulinda mali za raia wake.
Vikosi vya usalama vilipelekwa katika eneo hilo kwa ajili ya kuwasambaratisha wapiganaji hao
Shirika la habari la serikali ya Syria, SANA limesema kuwa wengi wa askari waliouawa walikuwa ni kutoka kwenye ngome iliyokuwa ya waasi ya Idlib.
Kulingana na SANA, wakati wa operesheni hiyo, vikosi vya usalama vilimkamata aliyekuwa mkuu wa ujasusi wa jeshi la anga, Jenerali Ibrahim Huweija. Jeshi hilo ni mojawapo ya vikosi vya usalama vinavyoaminika katika familia ya Assad.
Kutokana na mashambulizi hayo, Syria imeweka amri ya kutotoka nje kwenye maeneo yenye wakaazi wa jamii ya Alawi anakotokea Assad, ikiwemo Latakia, kwenye mji wa bandari wa Tartous, na Homs.
Uingereza yaondoa vikwazo dhidi ya Syria vya wakati wa utawala wa Assad
Katika hatua nyingine, Uingereza imeondoa vikwazo ilivyoweka wakati wa utawala wa Assad dhidi ya kampuni 24 ikiwemo Benki Kuu ya Syria.
Taarifa iliyotolewa na serikali ya Uingereza imeeleza kuwa mwezi uliopita, nchi hiyo ilisema kwamba mabadiliko yoyote ya vikwazo yanalenga kuwaunga mkono watu wa Syria katika kuijenga tena nchi yao na kuimarisha usalama na utulivu.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria imeipongeza hatua hiyo ya Uingereza, ikisema ni nzuri ambayo itachangia mchakato wa kuufufua uchumi wa Syria na kurejesha hali nzuri ya kisiasa.
Hata hivyo, mamia ya vikwazo bado vinaendelea dhidi ya watu binafsi na makampuni.