Kiongozi wa kikosi cha SSA auwawa mjini Tripoli
13 Mei 2025Vifaru na magari ya kivita yalionekana katika mji wa Tripoli siku ya Jumanne baada ya kuzuka mapigano yaliyotokea kutokana na ripoti kwamba kiongozi wa kikosi maalum cha usaidizi (SSA) Abdulghani Kikli, maarufu kama Ghaniwa ameuawa. Milio ya risasi ikasikika katikati mwa jiji la Tripoli na maeneo mengine ya mji mkuu huo wa Libya.
Kiongozi huyo, Abdulghani Kikli, ni kamanda wa kikosi hicho maalum cha usaidizi ambacho ni miongoni mwa makundi yenye nguvu na yenye silaha katika jiji la Tripoli.
Kikosi hicho cha SSA kiko chini ya Baraza la Rais lililoingia madarakani mwaka wa 2021 pamoja na Serikali ya Umoja wa Kitaifa (GNU) ya Abdulhamid Dbeibah kupitia mchakato unaoungwa mkono na Umoja wa Mataifa.
Soma pia: Makazi ya waziri mkuu wa Libya yashambuliwa
Kituo cha Huduma za Dharura na Msaada kimesema mpaka sasa miili sita imepatikana katika maeneo ya mapigano karibu na kitongoji cha Abu Salim. Ripoti zinaeleza kuwa kuna uwezekano kwamba Abdulghani Kikli, alivamiwa katika eneo hilo la Abu Salim ambalo limo kwenye wilaya ya kusini mwa mji mkuu wa Tripoli ambako ndiko makao makuu ya kundi lake lenye ushawishi mkubwa na silaha.
Eneo la Abu Salim ni mojawapo kati ya vitongoji 12 vinavyojumuisha mkoa wa Tripoli, ni kitongoji kikubwa zaidi chenye takriban wakaazi 380,000.
Wizara ya Mambo ya Ndani ya serikali ya Umoja wa Kitaifa, GNU, imetoa wito kwa raia wabakie majumbani kwa ajili ya usalama wao.
Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya (UNSMIL) umezitaka pande zote kusitisha mapigano mara moja na kurejesha hali ya utulivu, na umezikumbusha pande zinazopigana juu ya wajibu wao wa kuwalinda raia.
Soma pia: Mjumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya ajiuzulu
Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya (UNSMIL) umesema katika taarifa yake iliyochapishwa kwenye mtandao wa X kwamba unasikitishwa na hali mbaya ya usalama inayoendelea mjini Tripoli, pamoja na mapigano makali ya kutumia silaha nzito katika maeneo yenye wakazi wengi. UNSMIL, imesisitiza kwamba inaunga mkono juhudi za wazee wa jamii na viongozi kwa ajili ya kupunguza mivutano.
Libya, ni mzalishaji mkuu wa mafuta katika eneo la Bahari ya Mediterania, imekumbwa na migogoro tangu uasi wa mwaka 2011 ulioungwa mkono na Jumuiya ya Kujihami ya NATO. Pande zinazopigana ziliigawa nchi hiyo mnamo mwaka 2014 na kuwa na pande mbili za mashariki na magharibi.
Serikali ya Umoja wa Kitaifa (GNU) iliyo na makao yake makuu mjini Tripoli inatambuliwa kimataifa na upande wa kaskazini-magharibi ndio makao ya makundi hasimu yenye silaha ambayo yamekuwa yakipigana mara kwa mara.
Vyanzo: RTRE/AFP