Kiongozi wa kijeshi Gabon kugombea urais uchaguzi wa Aprili
4 Machi 2025Oligui alikuwa ameahidi kukabidhi madaraka kwa raia katika taifa hilo lenye utajiri wa mafuta la Afrika ya Kati baada ya kipindi cha mpito kufuatia kuondolewa kwa rais Ali Bongo Ondimba Agosti 2023. Lakini kanuni mpya ya uchaguzi iliyoidhinishwa na bunge la mpito mwishoni mwa Januari ilifungua njia kwa wanajeshi na mahakimu kugombea uchaguzi.
Katika hotuba yake kwenye mji mkuu Libreville Jumatatu, Oligui alisema, baada ya kutafakari kwa kina na kujibu maombi mengi ya wananchi, ameamua kuwa mgombea katika uchaguzi wa urais wa Aprili 12. Kiongozi huyo aliyefikisha umri wa miaka 50 jana, alisema maono yake ya muhula wa miaka saba madarakani ni "ya Gabon inayoinuka kutoka kwenye majivu", akiahidi kushughulikia masuala ya miundombinu ya nchi hiyo.
Ili kuwasilisha ombi lake, mkuu huyo wa zamani wa kitengo cha ulinzi wa rais lazima aache kwa muda sare yake ya kijenerali wakati akiwania uchaguzi. Baada ya kipindi cha uchaguzi, ataivaa tena sare ya kijeshi wakati akisubiri matokeo ambapo kama atachaguliwa, hatoivaa tena. Na asiposhinda uchaguzi, amesema aterejea jeshini.