Kiongozi mkuu wa upinzani Ivory Coast ajiuzulu uongozi
12 Mei 2025Kiongozi mkuu wa upinzani nchini Ivory Coast, ambaye amezuiwa kugombea uchaguzi wa rais utakaofanyika mwezi Oktoba, ametangaza kujiuzulu kama mwenyekiti wa chama chake cha Democratic (PDCI).
Tidjane Thiam hata hivyo amesema bado ataongoza mapambano ya kuutwaa ushindi katika uchaguzi ujao. Kampeni ya mwanasiasa huyo ya kugombea urais imegubikwa na mvutano kuhusu suala la uraia wake.Soma pia: Outtara asema yuko tayari kuendelea kuhudumu kama rais
Mahakama ya mjini Abidjan mwezi uliopita ilimuengua kwenye orodha ya wagombea urais ikisema amepoteza haki ya kuwa raia wa nchi hiyo baada ya kuchukua uraia wa Ufaransa mwaka 1987.
Wanasiasa wengine watatu wa upinzani akiwemo rais wa zamani Laurent Gbagbo pia walienguliwa huku rais wa sasa Alassane Ouattara, aliyeko madarakani tangu 2011, akiwa hajatangaza bado kugombea japo amesema ana hamu kubwa ya kuendelea kuitumikia Ivory Coast.