Kinshasa. Watu 26 wauwawa katika ghasia za maandamano mjini Kinshasa.
2 Julai 2005Kiasi watu 26 wameuwawa siku ya Alhamis wakati polisi katika jamhuri ya kidemokrasi ya Congo DRC walipovunja maandamano ya vyama vya upinzani katika miji kadha nchini humo.
Serikali imesema kuwa watu 10 wameuwawa wakati polisi walipovunja maandamano hayo ya wapinzani katika miji kadha . Chama kikuu cha upinzani cha Union for Democracy and Social Progress UDPS hapo mapema kilitoa idadi hiyo ya watu waliokufa , lakini jana Ijumaa ilitoa idadi mara mbili ya hiyo.
Joseph Mukendi msaidizi mkuu wa mkuu wa chama cha UDPS amesema kuwa watu sita wameuwawa katika mji mkuu Kinshasa na zaidi ya 20 wameuwawa katika majimbo makuu mawili ya kati ya Kasai. Maandamano hayo yamefanyika kupinga kushindwa kufanyika kwa uchaguzi kama ulivyopangwa chini ya makubaliano yaliyofikiwa kati ya serikali na makundi ya waasi mwaka 2003 ambayo yalimaliza vita vya miaka mitano nchini humo.